1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombeaji wakuu 2 wakubali kushiriki katika uchaguzi, Guinea.

21 Oktoba 2010

Guinea haijawahi kuwa na uchaguzi mkuu huru tangu 1958.

https://p.dw.com/p/Pjr0
Jenerali Sekouba Konate analiongoza Guinea katika serikali ya muda.Picha: picture-alliance/dpa

Wagombeaji wawili wa urais ambao ni mahasimu kisiasa nchini Guinea wamesema wako tayari kushiriki katika uchaguzi mkuu wa marudio Jumapili ijayo. Uchaguzi huo uliahirishwa baada ya mkuu wa tume ya uchaguzi katika nchi hiyo ilioko Afrika magharibi kuondolewa kutokana na tuhuma za kupendelea upande mmoja.

Kuteuliwa kwa afisa kutoka Mali aitwaye Siaka Toumany Sangare kuiongoza tume ya uchaguzi nchini Guinea kumepigiwa upatu na Ufaransa ambayo imetoa mwito kwa Guinea iliyokuwa chini ya ukoloni wake, kukamilisha uchaguzi wake wa kwanza huru tangu ilipojipatia uhuru mwaka wa 1958.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Bernard Kouchner aliutaja mwelekeo huo kuwa wa umuhimu mkubwa. Alisema kwamba amekuwa akiwasiliana na wagombeaji wawili wakuu, Cellou Diallo na Alpha Conde na wako radhi kushiriki katika uchaguzi uliopangwa kufanyika siku ya Jumapili.

Guinea Präsident Wahlen Kandidat Alpha Conde Flash-Galerie
Mgomeaji wa urais, Alpha Conde alipata asilimia 18 ya kura katika awamu ya kwanza ya uchaguzi mwezi Juni.Picha: AP

Hata hivyo haijajulikana ikiwa kusitishwa kwa mzozo wa uongozi katika tume ya uchaguzi kutatosheleza kuuokoa uchaguzi wa tarehe 24 mwezi huu kwa sababu sintofahamu hiyo ilisababisha kucheleweshwa kwa matayarisho na uchaguzi huo unaweza kuahirishwa tena.

Cellou Dallein Diallo amesema yuko tayari kushiriki katika uchaguzi huo. Bw Diallo ni waziri mkuu wa zamani na alikuwa amemnyoshea mkuu wa tume ya uchaguzi, Louceny Camara, kidole cha lawama akisema alikuwa akipendelea upande mmoja.

Foumba Kourouma ambaye ni afisa katika tume ya uchaguzi amesema tayari vifaa vya uchaguzi vimewasilishwa na vitasambazwa nchini katika muda wa siku mbili.

Mtaalam na mchunguzi wa masuala ya kisiasa katika shirika linalotathmini mizozo duniani, ICG Bw Mohammed Jalloh alionya kwamba haitakuwa jambo la busara kulazimisha uchaguzi huo ufanyike siku ya Jumapili kwa sababu mkuu wa tume hiyo mpya kutoka Mali anahitaji muda ili aweze kuidhibiti tume hiyo.

Uchaguzi huo katika taifa lililoko chini ya uongozi wa kijeshi na ambalo lina utajiri wa madini, unatizamwa kama nafasi nzuri zaidi ya kusitisha miongo ya uongozi wa kidikteta na pia kuondoa wasiwasi ambao umekuwepo tangu mapinduzi ya mwaka wa 2008.

Awamu ya kwanza ya uchaguzi nchini humo ilikamilika bila visa vya ghasia mwezi Juni licha ya malalamiko ya wizi wa kura na kukaripiwa kwa tume ya uchaguzi.

Guinea Präsident Wahlen Kandidat Cellou Dalein Diallo
Mgombeaji wa urais, Cellou Dallein Diallo aliwahi kuwa waziri mkuu nchini Guinea.Picha: AP

Na huku hayo yakijiri, zaidi ya watu 170 wamekamatwa kwa kuhusika katika ghasia wiki hii nchini Guinea. Duru za polisi zinasema kwamba waliokamatwa walikuwa wafuasi wa Bw Diallo waliokabiliana na maafisa wa polisi katika mji mkuu, Conakry ambapo watu wawili waliuawa na wengine 40 walijeruhiwa.

Mwandishi, Peter Moss /AFP /Reuters

Mhariri, Josephat Charo