Wagombea wakuu wa uchaguzi wa urais Kenya wapiga kura
9 Agosti 2022Mgombea urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga amepiga kura asubuhi ya leo katika kituo cha Old Kibera, jijini Nairobi. Raila ambaye ni mwanasiasa mkongwe, alikuwa ameongozana na mkewe, Ida Odinga.
Kwa upande wa naibu rais wa Kenya, William Ruto mwenye umri wa miaka 55, ambaye pia ni mgombea urais kupitia muungano wa Kenya Kwanza, yeye amepiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi ya Kosachei iliyoko katika eneo la Eldoret Kaskazini, kaunti ya Uasin Gishu, Bonde la Ufa.
Wagombea wengine wanaowania kiti cha urais ni George Wajackoyah wa chama cha Roots na David Mwaure wa chama cha Agano.
Utafiti wa maoni ya mpiga kura ulitabiri ushindani mkali kati ya Odinga na Ruto. Zaidi ya wapiga kura milioni 22 wamejiandikisha kushiriki uchaguzi wa Jumanne utakaohitimisha utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, huku asilimia 40 wakiwa na chini ya umri wa miaka 35.
Kuelekea uchaguzi huo mkuu, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC ilitangaza kuahirisha uchaguzi wa magavana wa Mombasa na Kakamega, kwa madai ya hitilafu katika karatasi za kupigia kura. Uchaguzi mwingine uliofutwa ni ule wa viti vya ubunge vya Kacheliba na Pokot Kusini.
Suala la kupanda kwa gharama za maisha, ufisadi uliokithiri ni miongoni mwa masuala yatakawasukuma wapiga kura. Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yatatangazwa ndani ya wiki moja baada ya uchaguzi.