Wagombea 15 Senegal wataka kura kabla ya rais kuondoka
19 Februari 2024Wagombea 15 kati ya 20 walioidhinishwa kugombea katika uchaguzi wa urais nchini Senegal, wametaka uchaguzi huo uliocheleshwa ufanyike kabla ya tarehe 2 Aprili, ikiwa pia ndio siku ambayo Rais Macky Sall atakamilisha muhula wake madarakani.
Taarifa ya kuahirishwa uchaguzi uliotakiwa kufanyika Februari 25, ilitangazwa masaa machache kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za wagombea. Hatua hiyo iliitumbukiza Senegal katika machafuko mabaya zaidi ya kisiasa kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.
Soma pia:Upinzani Senegal waongeza shinikizo Macky Sall
Wiki iliyopita, Mahakama Kuu ya Katiba ilibatilisha uamuzi wa kucheleshwa kwa uchaguzi huo. Wagombea hao wamesema inasikitisha kuona kwamba tangu uamuzi wa Baraza hilo la Katiba, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na mamlaka. Hata hivyo, bado kuna utata juu ya tarehe rasmi ya uchaguzi na pia orodha ya wagombea.