Wagiriki wapiga kura ya hasira
7 Mei 2012Katika uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili, wapiga kura wa Ugiriki walivipiga kumbo vyama vilivyokubali masharti ya kupatiwa mkopo ulioikoa nchi hiyo iliyokaribia kufilisika.
Matokeo haya yanaonyesha kuwa vyama vya New Democracy na kile cha mrengo wa kushoto cha Pasok vilikosa wingi wa viti vya kuviwezesha kuunda serikali baada ya kupata asilimia 32.1 tu kati yake. Idadi hii ni chini ya nusu ya viti vilivyopata vyama hivi ambavyo vimetawala siasa za Ugiriki kwa zaidi ya miongo minne, katika uchaguzi wa mwaka 2009.
Kura ya hasira
Badala yake, wapiga kura walionyesha hasira zao baada ya miaka miwili ya hali ngumu ya maisha kwa kuvichagua vyama vinavyopinga masharti ya mikopo kutoka Umoja wa Ulaya kwa kuvipa jumla ya viti 151 kati yake.
Matokeo haya ya kustukiza yanaiweka Ugiriki katika wakati mgumu sana kisiasa kwa kuwa mwanasiasa mashuhuri Antonis Samaras wa chama cha New Democracy itamuwia vigumu kuunda serikali atakapopewa jukumu hilo na rais baadaye leo.
"Tumeomba kupewa ridhaa ya nguvu, lakini raia wa Ugiriki wameamua vingine. Naheshimu maamuzi yao. Tuko tayari kuchukua jukumu la kuunda serikali ya kulinusuru taifa hili tukiwa na malengo makuu mawili--kubaki katika ya euro na kutafuta muafaka wa kisera katika namna ambayo itatuwezesha kuleta maendeleo na kuwapatia afueni wananchi," alisema Samaras.
Uwezekano wa kufanyika uchaguzi mpya
Kwa kuwa vyama vya Pasok na New Democracy ambavyo viliunda serikali inayomaliza muda wake iliyoongozwa na Waziri Mkuu Lucas Papademos, havitakuwa na wingi wa wabunge kuviwezesha kufanya maamuzi sasa, kuna uwezekano wa kufanyika uchaguzi mpya. Kibaya zaidi ni kwamba chama cha Pasok kimetupwa katika nafasi ya tatu, kikishindwa na chama mrengo wa kushoto cha Syriza ambacho kimepata asilimia 16.7 ya viti, mara tatu zaidi ya kilivyopata mwaka 2009.
Hatari ya kurudi kwa unazi
Kwa ujumla, vyama saba vimepata viti vya ubunge katika uchaguzi huu ikilinganishwa na vitano vilivyofanikiwa kuingia bungeni mwaka 2009. Hata chama cha kinazi cha Golden Down nacho kinatarajia kupata uwakilishi Bungeni tangu mwaka 1974 na kuwa chama cha sita kwa ukubwa katika Bunge hili la watu 300 kikiwa na wawakilishi 20.
Kiongozi wa chama hiki Nikos Michaloliakas alisema chama chake kitapigana dhidi ya alichokiita utumwa wa mikataba ya mikopo ya Umoja wa Ulaya na IMF ambayo aliifananisha na udikteta.
Vyama vya Pasok na New Democracy vimesema vinataka Ugiriki ifikiriwe zaidi kwenye mgao wa mkopo wa euro bilioni 240 unaotolewa na Umoja wa Ulaya, IMF na Benki Kuu ya Ulaya. Lakini kutokana na hasira za wapiga kura dhidi ya masharti ya mikopo hii ya kubana matumizi, vyama vidogo kikiwemo cha Syriza ambacho kinatizamwa kama mshirika katika kuunda serikali, vinataka mikataba hii iangaliwe upya.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\RTRE
Mhariri: Mohamed Khelef