Wageni wamiminika nyumba ya Mandela, Soweto
28 Juni 2013Wakati Mandela mwenyewe amelazwa hospitalini bado akiwa katika hali mbaya, watoto wa shule wa Afrika Kusini, hapo jana walijipanga katika foleni ndefu mbele ya nyumba ambamo Mandela aliishi hapo zamani katika kitongoji cha waafrika cha Soweto kilichopo Johannesburg. Mtoto mmoja ameeleza sababu ya kwenda kuitembelea nyumba hiyo akisema, "Yeye ni kama baba yangu. Nampenda Mandela. Nampenda sana."
Mwalimu wa watoto hao amesema wakati Mandela amelazwa hospitalini wameamua kwenda kwenye nyumba ya zamani ya Mandela, licha ya kuwa na mapumziko. Mwalimu huyo amesema watoto hao wenye umri kati ya miaka minane na kumi wanajifunza mengi juu ya Mandela shuleni. Lakini jee wanajua nini hasa juu yake. Mtoto mmoja amesema, "Yeye ndiye aliyetukomboa. Tumekuja hapa ili kumwonyesha jinsi tunavyompenda." Mtoto mwengine amesema, "Kwangu mimi Mandela ni shujaa kwa sababu aliupigania uhuru wetu."
Wajerumani hawajaachwa nyuma
Watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ikiwa pamoja na watalii wa kijerumani pia wanakendwa katika nyumba ya zamani ya Nelson Mandela. Msimamizi wa nyumba hiyo ambayo sasa imekuwa ya makumbuisho, Jane Monakwane, amesema idadi ya watu wanaoenda katika nyumba hiyo ya ukumbusho sasa imeongezeka. Patashika kubwa ya kuitembelea nyumba hiyo inaweza kufafanishwa na tukio la mwaka wa 1990 katika historia ya Afrika ya Kusini wakati ambapo Mandela, aliyekuwa mfungwa maarufu duniani alifunguliwa na kurejea katika maskani yake ya Soweto. Hata hivyo hakuendelea kukaa hapo kwa muda mrefu.
Mkuu wa makumbusho, Jane Monakwane, ameeleza kwa nini Mandela hakukaa katika nyumba hiyo kwa muda mrefu. "Nafikiri baada ya kuwamo kifungoni kwa miaka 27, Mandela hakutambua jinsi alivyogeuka kuwa mtu maarufu sana." Mandela alikaa katika nyumba yake ya Soweto kwa muda wa siku 11 pamoja na mkewe wa hapo zamani Winnie. Lakini kutokana na kusongwa na waandishi wa habari na watu wengine Mandela alihamia katika kitongoji cha watu wenye hali nzuri cha Houghton.
Watoto wa shule, wafanyabiashara na watalii wanaoitembelea nyumba ya Mandela ya Soweto pia wanaifuatilia hali yake wakati akiwa amelazwa hospitalini. Mtalii mmoja kutoka Ujerumani, Gisela Seemann, amesema ikiwa Mandela ni mgonjwa sana kiasi cha kusibika basi ni vyema lipatikane suluhisho. Lakini karibu na nyumba hiyo ya makumbusho pana bango la nembo ya kinywaji cha Whiskey; Johnny Walker, Yohana Mtembezi, likiwa na maana ya kumtakia Madiba uwezo wa kuendelea kutembea hadi afikie umri wa miaka 95.
Mwandishi: Schadomsky,Ludger
Tafsiri: Mtullya Abdu
Mhariri: Yusuf Saumu