1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WAGANDA WANAPIGA KURA LEO KUMCHAGUA RAIS NA WABUNGE

Abdu Said Mtullya18 Februari 2011

Watu wa Uganda leo wanapiga kura katika uchaguzi mkuu ambapo watawachagua Rais na Bunge jipya. Hata hivyo wachunguzi wanasema Rais wa hadi sasa Yoweri Museveni anatarajiwa kuchaguliwa tena.

https://p.dw.com/p/10JLO
Waganda katika uchaguzi mkuu.Picha: DW/Schlindwein

Watu wa Uganda wameshaanza kupiga kura kumchagua Rais na bunge jipya. Rais wa hadi sasa Yoweri Museveni anatarajiwa kuchaguliwa tena licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa wapinzani wakati wa kampeni za uchaguzi. Kwa mujibu wa kura za maoni, Museveni anaeitawala Uganda tokea mwaka wa 1986 anatarajiwa kuchaguliwa tena.

Hata hivyo mshindani wake mkuu, kiongozi wa upinzani Kizza Besigye ameshatoa madai juu ya wizi wa kura. Bwana Besigye pia mara kwa mara amesema panaweza kutokea upinzani kama ule wa nchini Misri ikiwa uchaguzi hautakuwa wa haki.

Uchaguzi wa leo ni wa tatu ambapo Museveni na mshindani wake mkuu Besigye wanakwenda sambamba. Chaguzi mbili za hapo awali zilimalizika kwa utatanishi kutokana na Besigye kujaribu bila ya mafanikio kuitaka Mahakama Kuu ya Uganda iyabatilishe matokeo.Kiongozi huyo wa upinzani safari hii anakusudia kuwaweka wasimamizi wake watakaozihesabu kura.

Rais Museveni na mpinzani wake mkuu Besigye ni wanasiasa waliokuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka mingi kabla ya kutofautiana na kuwa mahasimu.Besigye alikuwa daktari binafsi wa Rais Museveni wakati Rais huyo alipokuwa anaviongoza vita vya kutokea msituni dhidi ya utawala wa Uganda.

Besigye amesema kwamba safari hii hataenda mahakamani ,ikiwa matokeo hayatakuwa sawa na yale ya tume ya uchaguzi. Ametishia kutoa mwito kwa wananchi waishughulikie hali hiyo wao wenyewe moja kwa moja.

Hata hivyo wachunguzi wamesema upinzani kama ule wa Misri, siyo jambo linaloweza kutokea nchini Uganda.Kwa mujibu wa wachunguzi, huduma za mtandao wa Internet hazijaifikia sehemu kubwa ya wananchi,aidha kiwango cha elimu nchini Uganda siyo sawa na cha watu wa Misri.Mbali na hayo watu wa Uganda wanaliogopa jeshi lenye historia ya kutumia njia za mabavu kuzima upinzani.

Watu milioni 14 wanastahiki kupiga kura nchini Uganda.

Mwandishi Mtullya Abdu/RTRE/AFP/DW/

Mhariri/.....