Wagambia wapiga Kura
1 Desemba 2016Wananchi wa Gambia wanapiga kura katika uchaguzi wa rais ambao una ushindani mkali kati ya rais aliyeko madarakani Yahya Jameh ambaye ameitawala nchi hiyo kwa miaka 22 dhidi ya upinzani ambao umepata nguvu kubwa nchini humo. Licha ya umeme kukatika mapema leo shughuli ya kupiga kura ilianza bila matatizo katika nchi hiyo ambayo makundi ya haki za binadamu yamekuwa yakiituhumu serikali kwa kuukandamiza uhuru wa kutoa maoni.
Mshindi katika kinyang'anyiro hicho cha urais nchini Gambia kinachowakutanisha wagombea watatu atachukua uongozi wa kipindi cha muhula wa miaka mitano katika nchi hiyo ndogo iliyokuwa koloni la Muingereza katika eneo la Magharibi mwa Afrika ikipakana na Senegal.Mchezaji wa zamani wa soka wa kimataifa kutoka Gambia Alhaji Momodo akipiga kura asubuhi mjini Banjul amesema anamuunga mkono Jammeh kuendelea kuwa rais kwasababu amekuwa akifanya maendeleo makubwa katika nchi hiyo, Mchezaji huyo wa zamani wa soka ameendelea kusema kwamba anaamuamini rais Jammeh na hasa kwakuwa amekula kiapo kwa kitabu cha Quran kuitumikia Gambia na wananchi wake na kwenda kinyume na hilo mwenyezi mungu atamuadhibu.
Rais Jammeh anawania muhula wa tano madarakani pamoja na chama chake kinachotawala cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction APRC:Mgombea mwingine ni aliyekuwa mbunge wa chama tawala Mama Kandeh ambaye anasimama kupitia chama cha Democratic Congress GDC wakati mgombea wa tatu ni mfanyabiashara asiyejulikana sana Adama Barrow ambaye anaipeperusha bendera ya muungano wa kundi la vyama vya upinzani vilivyoshirikiana mara hii kwa mara ya kwanza na kuungwa mkono na raia wengi wa Gambia.
Rais Jammeh ameshatoa onyo kali kwa watu watakaojitokeza mitaani kuandamana kuyapinga matokeo ya uchaguzi huo akisema hilo jambo halitokubalika.Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limewatolea mwito maafisa wa serikali kuhakikisha kwamba kipindi cha uchaguzi na baada ya mchakato huo kitakuwa na utulivu na kuheshimiwa kikamilifu kwa haki zote za binadamu katika utoaji wa maoni yao..Inaarifiwa kwamba mawasiliano ya mtandao pamoja na simu yalizimwa katika mkesha wa uchaguzi huku mitandao mikuu ya mawasiliano kama whatsapp ,skype na Viber ikishindwa kufanya kazi.
Kutokana na hali hiyo upinzani umekuwa ukitegemea mawasiliano ya kutumiana ujumbe mfupi wa kawaida na kufanya mikutano yao pamoja na kuvuka viziuizi vya barabarani vilivyowekwa kila kona katika mji mkuu Banjul.
Imethibitika kwamba hakuna waangalizi wa kimataifa waliokwenda nchini humo kusimamia uchaguzi wamethibitisha pia wanadiplomasia lakini kuna kundi dogo la waangalizi wa Umoja wa Afrika pamoja na ujumbe wa Marekani na Ulaya wenye makao yake mjini Banjul.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Daniel Gakuba