Wafungwa kutoka Guantanamo wawasili Uruguay
8 Desemba 2014Watu hao sita ambao walisafirishwa kwa ndege ya jeshi la Marekani, ndio kundi kubwa zaidi kuwahi kuachiwa kwa pamoja kutoka gereza la Guantanamo Bay ambalo linashutumiwa na jumuiya. Wanne miongoni mwao ni raia wa Syria, mmoja ni kutoka Tunisia, na aliyebaki ni mpalestina.
Wote walituhumiwa kuwa wanamgambo wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida, lakini wameshikiliwa kwa muda wa miaka 12 bila kufunguliwa mashitaka yoyote. Tangu mwaka 2009 walikuwa wameondolewa mashitaka, lakini walibakia gerezani kwa sababu haikuwezekana kuwarejesha nyumbani kwao, huku Marekani ikihangaika kupata nchi ya kujitolea kuwapokea.Serikali ya Uruguay imethibitisha kuwasili kwa wafungwa hao bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.
Pango la wateka nyara
Rais wa nchi hiyo Jose Mujica amesema nchi yake imekubali kuwapokea watu hao kama wakimbizi kwa misingi ya kibinadamu, na kuahidi kuwa muda wowote watakapojisikia kuondoka nchini humo wanao uhuru wa kufanya hivyo mara moja. Rais Mujica pia ameikosoa Marekani na mfumo wake wa kuwaweka watu katika kizuizi cha Guantanmo.
''Lile sio gereza bali ni pango la wateka nyara. Gereza huwajibika kwa mfumo fulani wa sheria, na huwa na waendeshamashitaka wa aina moja au nyingine, na majaji wowote wale. Gereza pia huendeshwa kwa mfumo fulani wa sheria. Kule hakuna chochote.'' Amesema rais Mujica.
Alipochukua madaraka miaka sita iliyopita rais Obama aliahidi kulifunga gereza hilo, akisema limeitia doa sura ya Marekani machoni mwa dunia nzima. Hata hivyo muda huo wote ameshindwa kutekeleza azma yake hiyo, hasa kutokana na upinzani wa bunge la nchi yake.
Changamoto za kuifunga Guantanamo
Kwa wakati huu Marekani inawashikilia wafungwa wengine 67 ambao wameruhusiwa kuondoka, ambao hata hivyo kama wenzao sita waliopokelewa sasa na Uruguay hawana pa kwenda, wakihofia mashitaka iwapo watarudi katika mataifa yao, au wakihofia usalama wao.
Mjumbe wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Clifford Sloan ameisifu Uruguay na rais wake Jose Mujica kwa kile alichokiita ''uongozi wake imara wa kuwapa hifadhi watu ambao hawawezi kurudi kwao''.
Wakili wa mmoja wa wa watu hao waliopokelewa na Uruguay Ramzi Kassem amesema kwa kuwapokea watu hao kama binadamu huru, nchi hiyo ya Amerika Kusini imedhihirisha kwa vitendo, msimamo wake wa kishujaa.
Uruguay tayari imekwishawapokea wakimbizi wengine 42 kutoka Syria, na imesema itawapokea wengine 80. Mkurugenzi wa kituo cha kiislamu nchini Uruguay Tamar Chaky, amesema Uruguay imefanya ukarimu huo licha ya kwamba huenda ni nchi pekee ya Amerika Kusini isio ya msikiti hata mmoja.
Kwa wakati huu gereza la Guantanamo linabaki na wafungwa 136, ambayo ni idadi ndogo zaidi tangu lilipofunguliwa mwaka 2002. Mnamo siku 30 zilizopita Marekani imeweza kuwaondoa wafungwa wapatao 30 katika gereza hilo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre
Mhariri:Josephat Charo