1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Wafuasi wa Imran Khan wasitisha maandamano Pakistan

27 Novemba 2024

Chama cha waziri mkuu wa zamani wa Pakistan aliyeko gerezani Imran Khan kimeyasitisha maandamano katika mji mkuu Islamabad.

https://p.dw.com/p/4nTmP
Pakistan - Unruhen in Islamabad
Polisi wakifyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf mjini Islamabad, Jumanne, Nov. 26, 2024.Picha: Irtisham Ahmed/picture alliance/AP

Ni baada ya vikosi vya usalama kufanya ukandamizaji uliosababisha mamia ya wafuasi kukamatwa na wengine wakalazimika kukimbia. Maelfu ya wafuasi wa Khan wakiongozwa na mkewe walikusanyika Islamabad Jumatatu baada ya kuwasili kutoka ngome yake ya mkoa wa Khyber-Pakhtunkhwa, kaskazini magharibi, wakiapa kuishinikiza serikali imuwachilie huru. Waandamanaji walizusha vurugu na kuwauwa karibu maafisa sita wa usalama wakati wakielekea kukita kambi nje ya bunge. Maelfu ya polisi na jeshi walianzisha operesheni muda mfupi baada ya usiku wa manane kuyavunja maandamano hayo. Waziri wa Habari Attaullah Tarar amesema serikali ililazimika kuamuru msako mkali baada ya chama cha Khan cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) kuipinga serikali, akiongeza kuwa kilikuwa na mipango ya kulivamia bunge.Khan, aliyeiongoza Pakistan kati ya 2018 na 2022, amekuwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuhukumiwa kwa mashitaka kadhaa ya rushwa.