1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Vital Kamerhe waghadhabishwa na hukumu dhidi yake

Jean Noël Ba-Mweze16 Juni 2021

Chama cha UNC chake Vital Kamerhe nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hakijaridhika na kimesikitishwa na hukumu ya rufaa dhidi ya kiongozi wake.

https://p.dw.com/p/3v1nI
Kongo Vital Kamerhe
Picha: picture-alliance/dpa/T. Roge

Kamerhe ambaye ni Kiongozi wa zamani wa ofisi ya Rais Félix Tshisekedi alihukumiwa jana Jumanne miaka 13 jelani. Aliwahi kukata rufaa baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 mnamo Juni 2020 alipopatikana na hatia ya ubadhirifu wa fedha za umma zilizoandaliwa kununua majumba kwa mpango wa siku 100 wa rais Tshisekedi. 

Wafuasi wa chama cha UNC wamelaani kile wanachokiita hukumu ya mtu asiye na hatia, wakisisitiza kwamba Kiongozi wao amehukumiwa bila uthibitisho wa hatia.

Kinachowakasirisha ni kuona Vital Kamerhe anateswa gerezani licha ya hali ya afya yake kuzorota, akihukumiwa kuhusu majumba, ingawa baadhi ya majumba hayo yapo hapa nchini. Majumba mengine yapo bandarini katika nchi jirani. UNC haikubali hukumu hiyo ya kisiasa. 

 
Soma Pia: Mkuu wa ofisi ya rais wa DRC, Vital Kamerhe atiwa mbaroni
"Tuna huzuni kubwa sana kwa sababu tayari tumeona ya kwamba kuna mkono mweusi ambao unakuwa nyuma ya hii mambo. Wale ambao wanataka kumuondoa Vital Kamerhe ambaye alijitoa miaka yote kwa ajili ya Kongo, kumutia pembeni. Hatutawakubalia," amesema Delhomme Chubira, mmoja wa viongozi wa chama hicho.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo, Sammih Jamal mfanyabiashara mulebanon alikuwa amehukumiwa miaka 20, ila adhabu yake imepunguzwa hadi miaka sita. Na miaka mitatu ya Jeannot Muhima, mtumishi wa zamani wa ikulu ya rais ilipunguzwa hadi mwaka mmoja.

Upande mwengine, seneta Matata Ponyo, Waziri Mkuu wa zamani ameikwepa kesi ya ubadhirifu iliyokuwa imeandaliwa dhidi yake.

Rais Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe
Rais Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe

Kesi kuhusu fedha zilizokusudiwa mradi wa Kilimo wa Bukangalonzo na ambazo zilipotea wakati akisimamia mradi huo kama Waziri Mkuu. Lakini aliokolewa Jumanne na maseneta wenzake wakipiga kura dhidi ya kuondolewa kwake kinga za bunge.

"Hii pia ni fursa kwangu kuhakikisha kwamba sijawahi kuchukua hata dola moja toka fedha hizo. Kuhusiana na maadili yangu ya kazi, ingekuwa kuwakatisha tamaa wakongomani na waafrika wanaomini kuwa Waafrika wanao uwezo wa kusimamia mali ya umma," amesisitiza Matata Ponyo.

Ni maseneta 49 ndio waliopinga kupitia kura, kuondolewa kinga seneta Matata Ponyo. Wengine 46 walipiga kura ya kuunga mkono kinga za Matata kuondolewa ili afikishwe mahakmani. Yaani bwana Matata aliponea chupuchupu.