1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Rouhani waandamana Iran

30 Desemba 2017

Maelfu ya wafuasi wa serikali ya Rais Hassan Rouhani wa Iran wameandamana katika miji tofauti nchini humo kuiunga mkono serikali yao baada ya maandamano ya siku mbili ya kuwapinga viongozi wa kidini nchini humo

https://p.dw.com/p/2q8XZ
Iran Teheran Demonstrationen
Picha: Getty Images/AFP/H. Malekpour

Umati mkubwa wa wafuasi wa serikali ulikusanyika katika mji mkuu wa Tehran, Mashhad na miji mingine kuadhimisha kumbukumbu ya kumalizika kwa "uasi"- ikiwa ni vurugu za mwisho nchini humo zilizozuka baada ya uchaguzi wa 2009.

Serikali ya Iran imewaonya watu dhidi ya kufanya maandamano zaidi hii leo baada ya siku mbili za maandamano, yaliyochochewa na hasira kuhusiana na msururu wa matatizo ya kiuchumi.

"Tunawaomba wale wote wanaopokea miito hii ya kuandamana kutoshiriki katika mikutano hiyo inayokwenda kinyume na sheria kwa sababu watajiletea matatizo na pia kwa raia wengine," amesema Waziri wa Mambo ya Ndani Abdolrahman Rahmani Fazil.

Televisheni ya serikali IRINN imesema imepigwa marufuku dhidi ya kuripoti kuhusu maandamano hayo, yaliyonza Alhamisi katika mji wa pili kwa ukubwa wa Mashhad na kusambaa katika miji mingine.

Iran Proteste in der Stadt in Kermanshah
Maandamano ya kuipinga serikali mjini KermanshahPicha: peykeiran

Maandamano hayo awali yalikuwa ya kulalamikia matatizo ya kiuchumi, lakini kwa haraka yakageuka na kuwa ya kuupinga utawala huo kwa jumla. Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa "ulimwengu unatazama” baada ya waandamanaji kadhaa kukamatwa. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran Bahram Ghasemi amepuuzilia mbali matamshi ya Trump akiyataja kuwa yasiyo na maana. Vidio zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha mamia ya watu wakiandamana katika mji mtakatifu wa Qom Ijumaa jioni, huku watu wakisema kwa sauti kubwa "kifo kwa dikteta” na "waachilie huru wafunwga wa kisiasa”.

Picha za vidio zilionyesha maelfu ya watu wakiwa wamekusanyika katika miji ya Rasht, Hamedan, Kermanshah, Qazvin na kwingineko, huku polisi wakijibu kwa kutumia mizinga ya maji.

Maafisa wamelaumu shinikizo la kutoka nje kuwa chanzo cha maandamano hayo. Hata hivyo maafisa wameonya dhidi ya kuipuuza hasira ya umma iliyoshuhudiwa katika siku za karibuni. Mshauri wa rais Hassan Rouhani kuhusu masuala ya kitamaduni Hesamoddin Ashena, amesema kwenye Twitter kuwa nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa za ukosefu wa ajira, mfumko wa bei, rushwa, ukosefu wa maji, pengo la kijamii, pamoja na usambazaji wa bajeti usio na usawa

Tangu alipochukua madaraka katika mwaka wa 2013, Rais Hassan Rouhani amedhamiria kuisafisha sekta ya mabenki na kuufufua uchumi, lakini wengi wanasema hatua maendeleo hayo yanafaywa kwa mwendo wa polepole sana.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
MHariri: Yusra Buwayhid