Wafuasi wa Mursi waitisha maandamano
2 Agosti 2013Wito wa kufanyika maandamano hayo ya leo (02.08.2013), umetolewa wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry akisema kuwa hatua ya jeshi kumuondoa madarakani Mursi, aliyekuwa amechaguliwa kwa kuzingatia demokrasia, ilikuwa ni ombi la mamilioni ya Wamisri na huku wito wa kimataifa ukitolewa kwa polisi kuwataka wajizuie kutumia nguvu.
Matamshi hayo ya Kerry yametolewa hadharani kuonyesha jinsi Marekani inavyounga mkono mapinduzi ya Julai 3 mwaka huu, huku wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wakifanya mazungumzo na serikali ya mpito na wafuasi wa Mursi kwa lengo la kutafuta suluhu.
Wananchi waliomba msaada wa jeshi
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Pakistan cha Geo, Kerry amesema kuwa mamilioni ya Wamisri waliliomba jeshi kuingilia kati, kutokana na hofu ya nchi hiyo kutumbukia katika ghasia. Ameongeza kusema kuwa jeshi lilirejesha demokrasia na sio kuiendesha nchi kwa sababu sasa kuna serikali ya kiraia.
Msemaji wa muungano unaomuunga mkono Mursi na unaopinga mapinduzi hayo, Allaa Mostafa, amesema kuwa maandamano ya amani yataendelea. Wafuasi wa Mursi wamepuuzia wito uliotolewa awali na wizara ya mambo ya ndani kuhusu kuwalinda iwapo hawatoandamana, huku jeshi likijadiliana jinsi ya kurejesha hali ya utulivu kwa lengo la kumaliza maandamano.
Taarifa ya wizara ya mambo ya ndani ya Misri, iliwataka waandamanaji katika uwanja wa Rabaa al-Adawiya na Nahda kuondoka salama bila kufukuzwa. Nalo gazeti linalomilikiwa na serikali la Al-Ahram, limenukuu duru za kipolisi kwamba vikosi vya usalama vimeanda mpango wa kumaliza maandamano hayo.
Umoja wa Ulaya watoa wito wa kusitishwa maandamano
Wakati hayo yakijiri, juhudi za kidiplomasia za kumaliza mzozo nchini Misri na kuzuia umwagikaji zaidi wa damu zinaendelea. Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya katika Mashariki ya Kati, Bernardino Leon na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle wako mjini Cairo kwa lengo la kuzitaka pande zinazohasimiana kutafuta suluhu.
Afisa wa juu wa chama cha Freedom and Justice, ambacho ni tawi la chama cha Mursi cha Udugu wa Kiislamu, amesema kuwa wajumbe hao wa Umoja wa Ulaya wamewaomba waache kuandamana. Baada ya kukutana na wawakilishi wa Udugu wa Kiislamu, Westerwelle alionya kuwa hali nchini Misri ni tete.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amesema Marekani inahofia kutokea kwa ghasia zaidi na kwamba wana wasiwasi na mauaji ya wafuasi kadhaa wa Mursi yaliyotokea katika mapigano na vikosi vya usalama. Ameonya kuwa mauaji kama hayo kamwe hayakubaliki.
Ama kwa upande mwingine, balozi za Marekani za Abu Dhabi, Baghdad na Cairo, zitafungwa Jumapili ijayo ya tarehe 4 kutokana na sababu za kiusalama. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Marie Harf, amesema kuwa balozi hizo zitafungwa au shughuli zake kuahirishwa kwa siku hiyo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman