1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Lula da Silva wamtaka asikubali kukamatwa

Sylvia Mwehozi
6 Aprili 2018

Rais wa zamani wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, amepewa saa 24 kujisalimisha kwa polisi na kuanza kutumikia kifungo cha miaka 12 kwa makosa ya ufisadi.

https://p.dw.com/p/2vcy4
Luiz Inacio Lula da Silva
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Peres

Hata hivyo wafuasi wake wamemshauri asikubali kukamatwa. Lula ni mmoja wa wanasiasa waliokuwa wanatarajiwa kutoa ushindani mkali katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini humo.

Agizo la mahakama lilimpa Lula saa 24 pekee kujisalimisha, hatua ambayo imewashangaza mawakili wake ambao walikuwa wanatarajia kuwa angepelekwa gerezani juma lijalo.

Lula, alishtakiwa mwaka uliopita kwa kupokea jumba kando ya bahari kama rushwa. Jumatano alijaribu kuishawishi mahakama ya Juu kumuachia huru huku akijaribu kukata rufaa akiendelea kufanya kampeni kwa uchaguzi muu ujao.

Umati wa kiasi wafuasi 2000 waaminifu wa chama cha Wafanyakazi, walisimama nje ya jengo kubwa karibu na mji wa Sao Paulo wakiapa kuwa hawatukabali polisi kumkamata Lula.

Brasilien Demonstration Lula da Silva
Shabiki wa rais wa zamani Lula da Silva Picha: Getty Images/AFP/C. de Souza

 Kuhusu kadhia hiyo liyekuwa rais wa Brazil Dilma Rousseff amesema, "wanataka kubadilisha na kufuta historia ya miaka 13 ya yale tuliyofanikisha Brazil tulipokuwa afisini.” Lula, mwenye umri wa miaka 72, leo asubuhi alipunga mkono dirishani ndani ya jumba lake la orofa lakini hakuzungumza na umma.

Taswira ya matukio imebadilisha mkondo wa matukio ya kisheria na kuzima nia na matumaini ya kiongozi huyo mkongwe kuwania kiti cha urais katika uchaguzi utakaoandaliwa mwezi wa Oktoba licha ya kura ya maoni kuonyesha kuwa anaongoza.

Admir da Jose mwenye umri wa miaka 57, anasema kuwa Lula lazima akatae kutiwa nguvuni hadi mwisho. anaongeza kusema kuwa Lula hatakimbia kokote, atakaa hapa na hawatamsalimisha bila ya makabiliano.

Mapema jaji Sergio Moro, anayeongoza uchunguzi dhidi ya ufisadi nchini Brazil alikuwa ameagiza Lula kujisalimisha mwenyewe kwa hiari kwa polisi katika mji wa kusini wa Curitiba kufikia saa kumi na moja saa za asubuhi saa za Brazil.

Brasilien Oberster Gerichtshof verhandelt über Haft von Ex-Präsident Lula | Präsidentin Carmen Lucia
Jaji wa mahakama ya juu Carmen Lucia nchini BrazilPicha: Reuters/A. Machado

Moro aliongeza kusema kuwa, kutokana na hadhi ya Lula, gereza maalumu lilikuwa limetayarishwa kwa ajili yake mapema. Chumba cha gereza la rais huyo wa zamani kimetengwa na wafungwa wengine.

Katika kesi iliyosikilizwa kwa muda mrefu, mahakama ilitoa uamuzi Alhamisi ambao ulidhihirisha kuwa Lula atafungwa.

Kuondolewa kwa Lula kwenye kinyang'anyiro cha urais kutaweka wazi ugombeaji wa kiti hicho. Kwa sasa aliyekuwa afisa wa jeshi mwenye msimamo mkali Jair Bolsonaro, ambaye hushangilia utawala wa kiimla wa Brazil kati ya mwaka 1964-1985 ni wa pili kwenye kura ya maoni.

Lakini Lula, aliyekulia katika umaskini bila ya elimu ya kutosha na kuwa kiongozi wa miungano ya wafanyikazi amesema ataendelea kupigana licha ya hali inayomkabili.

Alipoondoka afisini baada ya kuhudumu kwa kipindi cha mihula miwili mwaka 2011, alikuwa miongoni mwa viongozi ulimwenguni waliooredheshwa kuwa na viwango vizuri vya utendajikazi.

Kimsingi yeyote anayehukumiwa na kupoteza kesi kwenye mahakama ya rufaa nchini Brazil hawezi kugombea kwa mujibu wa sheria za taifa hilo.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Afp

Mhariri: Josephata Charo