1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Dilma Rousseff kuandamana

Grace Kabogo31 Machi 2016

Watu wanaomuunga mkono Rais wa Brazil Dilma Rousseff wanapanga kuingia mitaani kwenye miji mbalimbali kwa lengo la kulishinikiza bunge kabla ya kufanyika kura ya kutokuwa na imani na kiongozi huyo.

https://p.dw.com/p/1IMYf
Waandamanaji wamuunga mkono Rais wa Brazil Dilma Rousseff
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Peres

Wafuasi wanaoiunga mkono serikali ya Brazil na chama cha mrengo wa kushoto cha Wafanyakazi, wameitisha maandamano kwenye miji 31 ya nchi hiyo, huku maandamano makubwa yakitarajiwa kufanyika kwenye mji mkuu, Brasilia, na yataongozwa na rais wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva.

Lula ambaye ni mwanzilishi wa chama tawala cha Wafanyakazi na anayeendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho, amewataka wafuasi wa chama hicho kuingia mitaani. Wito huo aliutoa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa mawasiliano ya kijamii wa Facebook.

Jumatano Rais Rousseff alisema amekuwa muhanga wa jaribio la mapinduzi, wakati anapoendelea kupambana kushikilia nafasi yake serikalini, baada ya chama mshirika kujiondoa kwenye serikali ya muungano pamoja na kuongezeka kwa shinikizo la bunge kuitisha kura ya kutokuwa na imani naye.

''Kuondolewa madarakani bila ya kutenda uhalifu wowote, hayo ni mapinduzi. Tunataka uchumi wa Brazil urejee kwenye mstari, bila ya kuwepo utulivu wa kisiasa, hatuwezi kufanikiwa. Wale wanotaka kuingilia kati serikali iliyochaguliwa kihalali, bila kutumia njia za kisheria, watawajibika kwa kuchelewa kuimarika na kukua kwa uchumi na kupatikana kwa ajira,'' alisema Rousseff.

Waziri wa michezo ajiuzulu

Kiongozi huyo anaonekana kama ametengwa baada ya chama cha PMDB kutangaza kinajiondoa kwenye serikali ya muungano na kwamba kitaunga mkono kura ya kutokuwa na imani na Rousseff.

Waziri wa michezo Brazil George Hilton © Getty Images/E. Sa
Waziri wa michezo Brazil George HiltonPicha: Getty Images/E. Sa

Hayo yanajiri wakati ambapo mzozo wa kisiasa unazidi kuongezeka baada ya Waziri wa Michezo wa Brazil, George Hilton kujiuzulu wadhifa wake, miezi mitano kabla ya kuanza kwa michezo ya Olimpiki katika majira ya joto mjini Rio de Janeiro. Hilton amejiuzulu japokuwa sio mwanachama wa PMDB.

Nafasi ya Hilton itashikiliwa kwa muda na Ricardo Leyser, afisa katika wizara ya michezo, ambaye amekuwa akiratibu mchakato mzima wa maandalizi ya michezo hiyo kati ya serikali ya Brazil na kamati ya michezo ya Olimpiki. Hata hivyo, haijajulikana Leyser ataishikilia nafasi hiyo kwa muda gani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon ameelezea wasiwasi wake kuhusu mzozo wa kisiasa nchini Brazil. Ban ameliambia gazeti la O Estado de Sao Paulo kwamba mzozo wowote wa kisiasa nchini humo ni sababu inayopaswa kutiliwa wasiwasi.

Shinikizo la kumtaka Rais Rousseff aondoke madarakani, linatokana na madai kwamba alikiuka masharti ya bajeti ya mwaka 2014, ili kuukoa uchumi wa nchi hiyo usiporomoke, ikiwemo kashfa kubwa ya rushwa dhidi ya kampuni ya mafuta ya Petrobras.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga