1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi wenye vyeti bandia kufutwa kazi Tanzania

Zulfa Mfinanga28 Aprili 2017

Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamuru kufutwa kazi kwa watumishi zaidi ya 9,000 wa serikali yake kwa wakati mmoja hivi leo, muda mchache baada ya kupokea ripoti ya watumishi wa umma ambao vyeti vyao vilikuwa na utata ikiwamo kufojiwa.

https://p.dw.com/p/2c6Gl

Akikabidhi ripoti hiyo katika Chuo Kikuu cha Dodoma mchana wa leo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Anjela Kairuki, alisema katika uchunguzi wao wamebaini pia vyeti zaidi ya 1,500 vinatumika na watumishi zaidi ya mmoja kwa kila cheti na kwamba uchunguzi dhidi yao unaendelea.
Kwa mujibu wa ripoti kuhusu uchunguzi, watumishi wa umma zaidi ya watumishi elfu tisa walibainika kughushi vyeti na kupewa kazi kinyume na taratibu. Na punde tu, baada ya kukabidhiwa rasmi ripoti hiyo, Rais Magufuli alitangaza kuwa kuanzia leo amewafuta kazi watumishi hao na kuahidi kuendelea na uchunguzi kwa awamu nyingine.
Hatua yakosolewa
Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi wa umma kwenye mji mkuu wa Tanzania, Dodoma, ambapo ripoti hiyo imekabidhiwa, wanasema  kuwa zoezi hilo limekuja kwa kuchelewa kwani watumishi hao wamechangia kuzorotesha maendeleo ya nchi kwa kiasi kikubwa. Josephine Manase ni mmoja wao:
Mbali na kuagiza kufutwa kazi kuanzia leo kwa watumishi wote waliokumbwa na kashfa hiyo, rais huyo anayetambuliwa kwa hatua zake za kushitukiza na matamko ya hadharani, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa watumishi hao kujisalimisha vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Amewaahidi wale watakaojisalimisha kuwa watasamehewa na hawatofikishwa mahakamani. 

Hata hivyo, kinyume na ilivyotazamiwa na wengi, msako huo wa kubaini vyeti bandia haukuwahusisha watendaji wa serikali wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya, mawaziri na hata wabunge na madiwani, kwa kile ambacho kimetajwa kuwa wao si watumishi wa umma, bali wanasiasa. 

Hivi karibuni Serikali ya Tanzania pia iliendesha operesheni ya kuwatambua watumishi hewa na kubaini kuwa zaidi watumishi 19,000 walikuwa hawako kazini.

Nikiripoti kutoka hapa Dodoma kwa niaba ya DW, mimi ni Zulfa Mfinanga

Mwandishi: Zulfa Mfinanga
Mhariri: Mohammed Khelef