Wafanyakazi wa soko la Kariakoo wagoma, Dar es Salaam
15 Mei 2023Mgomo huu ambao unaweza kuathiri maeneo mingine ya kibiashara unachukuliwa na wafanyabiashara hao kama shinikizo kwa serikali wakiitaka iyatafutie ufumbuzi masuala kadhaa kikiwamo kiwango kikubwa cha kodi kinachotozwa na Mamlaka ya Mapato nchini, TRA.
Masuala mengine yanayotajwa ni kunyanyaswa na vyombo vya dola kama vile kukamatwakamatwa, kutokuwepo kwa mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara pamoja na mlolongo mrefu wa utoaji mizigo bandari.
Licha ya juhudi za mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, aliyefika katika eneo hilo kuwasihi, wafanyabiashara hao wanaonekana kuweka ngumu.
Wafanyabiashara wataka suluhu ya haraka ichukuliwe kusawazisha suala hilo.
Wafanyabiashara hao wanasisitiza kuwa hawako tayari kuyafungua maduka yao hadi pale masuala hayo yatakapotiliwa maanani na wanakwenda mbali zaidi wakitaka Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati.
Tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imeshatangaza kwamba Waziri Mkuu Kasim Majaliwa yuko tayari kukutana na wafanyabiashara hao keshokutwa Jumatano ili kusikiliza malalamiko yao.
Soko la Kariakoo ni mojawapo ya masoko makongwe na yanayotegemewa sana hasa kutokana na kiungo muhimu cha kibiashara katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Mbali na hilo, soko hilo limekuwa likitumika kusafirisha mizigo na bidhaa katika mataifa mengine ya jirani kama vile, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia.
Mwandishi: George Njogopa