1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wademocrat watoa wito rasmi ili Trump aondolewe madarakani

11 Januari 2021

Wademocrat waapa kuendelea kushinikiza Rais Donald Trump aondolewe madarakani katika siku za mwisho za utawala wake, kufuatia tukio la wiki iliyopita ambapo wafuasi wake walivamia majengo ya bunge mjini Washington.

https://p.dw.com/p/3nlTq
USA Präsident Donald Trump
Picha: Saul Loeb/AFP

Wapo baadhi ya wanachama wa Republic ambao pia wanaunga mkono wito huo. 

Huenda Rais Trump akakabiliwa na mchakato wa pili wa kihistoria wa kutimuliwa kwake madarakani kabla ya muda wake kumalizika rasmi ofisini Januari 20, ambapo Joe Biden ataapishwa kama rais mpya.

Spika wa baraza la wawakilishi katika bunge la Marekani Nancy Pelosi, amesema watawasilisha rasmi Jumatatu azimio kulitaka baraza la mawaziri kumuondoa Trump kwa msingi kuwa hafai kuwa ofisini chini ya ibara ya 25 ya katiba ya Marekani.

Pelosi: Tumia ibara ya 25, au mchakato uanze bungeni

Pelosi ameongeza kwamba ikiwa makamu wa rais Mike Pence hatatumia ibara hiyo, basi watawasilisha hoja ya kikatiba bungeni ili atimuliwe. ”Kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo hofu ya kushambuliwa kwa demokrasia kutokana na uchochezi wa rais inavyozidi kuongezeka, kwa hivyo kuna haja ya hatua kuchukuliwa.” Amesema Pelosi.

Spika wa bunge nchini Marekani
Spika wa bunge nchini Marekani Picha: Erin Scott/REUTERS

Soma pia: Twitter yafunga kabisa akaunti ya Rais Trump

Alipoulizwa ikiwa muda upo kweli wa kutosha wa kumtimua Trump kupitia mchakato wa bungeni alijibu akisema:

"Ninapenda ibara ya 25 kwa sababu inamuondoa moja kwa moja na atakuwa nje ya ofisi. Lakini kuna uungwaji mkono mkubwa bungeni wa kutimuliwa kwake kupitia mchakato wa bungeni kumuondoa rais kwa mara ya pili."

Mnamo Disemba 2019, Trump alipigiwa kura ya kuondolewa madarakani na bunge hilo la wawakilishi linalodhibitiwa na Wademocrat kufuatia hatua ya kumshinikiza rais wa Ukraine kufichua maovu ya kisiasiasa ya Biden.

Kisiki cha muda mfupi uliosalia na udhibiti wa seneti

Hata hivyo baraza la seneti linalodhibitiwa na Warepublic lilimuondolea mashtaka hayo.

Japo muda unazidi kuyoyoma, huenda Wademocrat wakapiga kura kumuondoa Trump madarakani, hatua ambayo inaweza kutapata uungwaji mkono kutoka kwa Warepublican wengi wanaounga mkono wito huo.

Hata hivyo kuna uwezekano watakosa wingi wa theluthi mbili unaohitajika ili kufanikisha mashtaka dhidi ya Trump katika baraza la seneti lenye wanachama 100 ndipo wamuondoe madarakani.

Seneta wa chama cha Democratic Chuck Schumer
Seneta wa chama cha Democratic Chuck SchumerPicha: US Senate Television/CNP/ZUMA Wire/imago images

Wito kwa Trump kujiuzulu

Seneta wa chama cha Republic Pat Toomey, ameliambia kituo cha televisheni cha Marekani CNN kwamba, kujiuzulu ndio njia nzuri kwa Trump kuacha madaraka.

Toomey amesema kuwa tangu Trump aliposhindwa kwenye uchaguzi wa Novemba 3, amejihusisha na matukio ya kushangaza ambayo hayakufikirika na yasiyosameheka.

Soma pia: Trump asema hatohudhuria kuapishwa kwa Biden

Lisa Murkowski ambaye ni seneta wa Republic kutoka jimbo la Alaska, ndiye alikuwa wa kwanza katika chama hicho cha Trump kumtaka ajiuzulu, wito ambao umetolewa pia na seneta Adam Kizinger.

Kitisho cha vurugu kuelekea uapisho wa Biden

Seneta wa chama cha Democratic Chuck Schumer ameonya kwamba bado kuna kitisho kikubwa cha vurugu kutoka kwa makundi yenye misimamo mikali, baada ya uvamizi wa majengo ya bunge uliofanywa na wafuasi wa Rais Trump.

Kwenye taarifa, Schumer amesema amezungumza na mkurugenzi wa idara ya upelelezi FBI Christopher Wray kumhimiza kuongeza juhudi katika kuwafuatilia waliohusika na uvamizi huo.

Schumer amesema wiki chache zijazo ni muhimu katika mchakato wa demokrasia nchini humo kufuatia matarajio ya kuapishwa kwa Biden na Harris.

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

Polisi wawasaka waliohusika na vurugu Washington

Maafisa nchini Marekani wanaendelea kuwafuatilia wafuasi wa Trump waliohusika kwenye vurugu na uvamizi wa majengo ya Bunge, kwa lengo la kuwakamata na kuwafungulia mashtaka.

Maazimio ya kumuondoa Trump madarakani yanatarajiwa kuwa na mashtaka ya kuchochea vurugu zilizosababisha vifo vya watu watano.

Usalama wa majengo ya bunge Capitol Hill umeimarishwa mnamo wakati watu wenye misimamo mikali wametishia kuchukua hatua mpya siku zijazo mjini Washington na katika miji mingine mikubwa.

(AFPE)