1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WADA yaipa Kenya muda zaidi kutunga sheria

9 Aprili 2016

Ndoto ya wanariadha Kikenya kwenda Rio de Janeiro ipo hai, baada ya Shirika la Kimataifa la Kupambana na Dawa za Kuongeza misuli nguvu – WADA kuipa Kenya muda wa mwisho kabisa wa Mei 2 kutunga sheria

https://p.dw.com/p/1ISSO
China Leichtathletik WM in Peking - Männer 1500m - Asbel Kiprop
Picha: Getty Images/A. Lyons

Kenya wiki iliyopita, ilikosa kutimiza muda wa mwisho wa pili uliowekwa mwaka huu, wakati kamati huru ya kuangalia uzingatiaji wa sheria hizo iliamua kuwa mpango wa Kenya wa kupambana na dawa za kuongeza misuli nguvu hauzingatii sheria za kimataifa.

Ikiwa Kenya haitapitisha sheria ya kufanya iwe uhalifu matumizi ya dawa hizo zilizopigwa marufuku michezoni na kuidhinisha rasmi sheria za shirika lake jipya la kitaifa la kupambana na dawa hizo ifikapo mwezi ujao, kamati ya mapitio itaiambia bodi ya WADA kuitangaza Kenya kuwa nchi isiyozingatia viwango hivyo.

Hatua hiyo imewatia moyo maafisa wa Kenya pamoja na wanariadha akiwemo bingwa wa dunia katika mchezo wa kurusha mkuki Julius Yego ambaye amesema sasa ni jukumu la serikali kuiharakisha sheria hiyo. "Nataka kusema serikali inapaswa kuchukua hatua ya haraka na kupitisha mswada huo ili kila kitu kiende sawa. Wakati tukijiandaa, hatutaki hali ambayo labda baadhi ya watu watasema Kenya itapigwa marufuku. Nataka wakati nikishiriki mashindanoni, kila mtu afahamu kuwa Kenya inazingatia sheria na sio kama baadhi ya nchi ambako kumekuwa na matatizo ya kutozingazia sheria hizo"

Julius Yego Speerwerfen Rom Italien Leichtathletik IAAF Diamond League 2015
Julius Yego, bingwa wa Dunia wa kurusha mkukiPicha: picture-alliance/dpa/G.Chai von der Laage

Waakti huo huo, Bodi ya maadili ya Shirika la Kimataifa la Riadha – IAAF imepinga ombi la Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Riadha Kenya la kupinga kusimamishwa kazi kwake kwa muda kutokana na tuhuma za kuitisha honfo kutoka kwa wanariadha wawili.

Isaac Mwangi alisimamishwa kazi kwa muda mwezi Februari, baada ya kuripotiwa madai hayo kutoka kwa wanariadha Joy Sakari na Francisca Koki Manunga. Mwangi alipinga uamuzi huo mwezi Machi.

Akizungumza katika ofisi yake mjini Nairobi, Sharad Rao, mpelelezi aliyeteuliwa na IAAF nchini Kenya, amesema amemfahamisha rasmi mtuhumiwa na mawakili wake kuwa sasa “anachukua rasmi uchunguzi kuhusiana na Isaac Mwangi ”ilifahamishwa kuwa Isaac Mwangi alipinga rasmi uamuzi wa kusitishwa kazi na akawasilisha ombi kwa bodi ya maadili ya IAAF la kutaka adhabu hiyo iondolewe. Suala hilo lilisikilizwa, naamini Isaac Mwanfi aliwakilishwa na mawakili na pia akawasilisha taarifa kadhaa kuunga mkono hoja zake kuwa hana hatia ya madai yaliyotolewa dhidi yake. Sasa nafahamu kuwa IAAF imetoa taarifa rasmi kuwa ombi hilo limetupiliwa mbali na hivyo adhabu bado ipo".

Sakari na Manunga wanatumikia adhabu ya kufungiwa miaka minne baada ya kugunduliwa kutumia dawa za kuongeza misuli nguvu wakati wa mashindano ya ubingwa wa dunia mwaka wa 2015.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/Reuters/DPA
Mhariri: Sessanga Iddi