1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachunguzi wa UA walaani uchaguzi wa Zimbabwe

Kalyango Siraj30 Juni 2008

Tsvangirai ataka Mugabe atengwe kisiasa

https://p.dw.com/p/ETf3
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, wakati wa kuapishwa katika ikulu mjini Harare Jumapili, Juni, 29, 2008.Picha: AP

Uchaguzi wa mwishoni mwa juma ambao umemrejesha madarakani rais Robert Mugabe unaendelewa kulaaniwa na kuitwa usiokuwa wa kidemokrasia na watu pamoja na makundi mbalimbali ndani na nje ya nchi hiyo.

Kundi la sasa kulaani ni ujumbe wa wachunguzi kutoka Umoja wa Afrika.

Ujumbe wa wachunguzi wa Umoja wa Afrika umetoa taarifa ukilaani uchaguzi wa Ijumaa.Uchgauzi huo ambao ulisusiwa na kiongozi wa upinzani Morgen Tsvangirai kutokana na madai ya vitisho dhidi ya wapinzani wake,na matokeo yake ni kuchaguliwa tena kwa bw Mugabe,umetajwa kama ambao haukuwa wa kidemokrasia.

Katika ripoti ya mwanzo ya ujumbe huo wa watu 40, umesema kuwa umeudhika na ghasia,vitisho pamoja na vyombo vya habari kuegemea upande mmoja.

Licha ya miito mbalimbali kwa vyama husika yaani chama cha rais Mugabe cha ZANU PF na kile cha mpinzani wake Tsvangirai cha Movement for Democratic Change MDC kukaa katika meza moja kujadialana,Umoja wa Afrika umesema kuwa umepewa moyo na utayarifu wa pande zote mbili husika wa kufanya mazungumzo.

Ingawa kulikuwa na taarifa za watu kulazimishwa kumpigia kura rais Mugabe,lakini ripoti ya Umoja wa Afrika inasema kuwa mambo yalikuwa salama katika siku ya kupiga kura na kuambatana na sheria za Zimbabwe za uchaguzi.

Hata hivyo ripoti hiyo imekosoa kile ilichokiita "vitisho" vilivyopelekea wapiga kura wasiteremke kwa wingi vituoni pamoja na kutokuwepo hali ya usawa katika kutumiwa vyombo vya habari vya serikali.Hali hiyo,ripoti inasema "imeutia dosari uchaguzi na kuufanya usiwe wa kidemokrasi."

"Kutokana na ila hizo na muongozo wa Umoja wa Afrika kuhusu chaguzi za kidemokrasi barani Afrika,tume ya uchunguzi ya Umoja wa Afrika inahisi uchaguzi wa Zimbabwe haumbatani na kanuni zinazokubaliwa na Umoja wa Afrika."

Ripoti hiyo imetangazwa mjini Harare katika wakati ambapo rais Robert Mugabe yuko Sharm el Sheikh nchini Misri ulikofunguliwa hii leo mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika unaogubikwa na mzozo wa Zimbabwe.

Serikali kadhaa za Afrika zinamshinikiza rais Mugabe asitawale peke yake,ajaribu badala yake kukishirikisha pia chama cha upinzani cha MDC.

Katika sherehe za kuapishwa hapo jana,aligusia uwezekano wa kuendeleza mazungumzo pamoja na MDC kwa lengo kupunguza tofauti zao.

Wafuasi wa MDC wamejibu kwa tahadhari wakisema "ni shida kuleta uwiano kati ya anachokisema na matumizi ya nguvu yanayoendelea."Hata hivyo MDC wamesema ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo ,utakaopelekea kuitishwa uchaguzi huru na wa haki ndio njia pekee ya kumaliza mzozo."

Hakuna wachunguzi wa mataifa ya magharibi waliokubaliwa kuchunguza uchaguzi huo.Ila Umoja wa Afrika ulikuwa na makundi matatu pamoja na bunge la Afrika na vilevile jumui ya SADC.

Ujumbe wa SADC wa watu 400 ulitoa taarifa yake jumapili ukisema kuwa kulitokea visa vya ghasia na haukutoa sura kuwa huo ni uamuzi halali wa wananchi.