Wachoraji wa katuni wanavyomwona Merkel
Wachoraji wa katuni kutoka duniani kote wanaonyesha namna wanavyomchukulia kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Kiongozi wa wapiga sarakasi
Wote wanafuata amri yake: Ugiriki na Uhispania mara nyingi zimefuata masharti ya Merkel, hadi ikawa kama vile zimepoteza nguo zote. Hata Italia iko karibu kupoteza suruali na bado muda mdogo hadi Ureno nayo idhalilishwe. Nchi za Ulaya ya Kusini zinamchukulia Merkel kama mtu anayesimamia mikakati yote ya uokozi wa sarafu ya Euro. (Uhispania, "Jarida Nonada")
Hakuna marafiki Athens
Hivi sasa Merkel ni mwanasiasa anayechukiwa zaidi Ugiriki. Raia wa nchi hiyo wanamlaumu kwa sababu ya uchumi wao unaoporomoka na kuongezeka kwa umasikini. Wagiriki wanasema kuwa Merkel amewafunga wote minyororo ilimradi aweze kuiokoa sarafu ya Euro. Kila mara Merkel anapokuja ziarani Ugiriki maandamano hufanyika. (Ugiriki, "To paron")
Mpanda farasi anayeleta mauti
Benki kuu ya Ulaya, Shirika la Fedha Duniani (IMF), waziri mkuu wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, na Angela Merkel wamepanda makopo yenye umbo la nguruwe ambayo hutumika kuweka akiba ya fedha. Ingawa Merkel anatabasamu, anajua namna ya kutumia upanga wake. Wakaazi wa Ulaya wanakubaliana juu ya suala hilo. (Ureno, "Expresso")
Furaha ya mzazi?
Katika nchi za Ulaya ya Kaskazini Merkel hachukuliwi kama tishio. Hilo halishangazi kwani sarafu inayotumiwa huko ni Krona na si Euro. Badala yake raia wa Sweden wanamwonea huruma Angela Merkel. Akiwa kama mama nguruwe ana vitoto vinane anavyotakiwa kuvinyonyesha na kuna cha tisa kinachonyemelea. Haelekei kuwa na furaha. (Sweden, "toonpool")
Njia panda kwa Ujerumani
Habari za mgogoro wa sarafu ya Euro zimefika hadi India. Nchi hiyo yenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Asia inachukulia kwamba uchumi wa Ulaya umeshazama. Ujerumani ni nchi pekee ambayo ingeweza kujiokoa na kuishi katika kisiwa. (India, "Kakanad, Kerala")
Amezidiwa ujanja
Baadhi ya wananchi wa Afghanistan wanasema kuwa Merkel anaamini mambo kwa haraka mno. Kansela huyo wa Ujerumani anaamini amani inaweza kurejea na hivyo ananunua silaha kutoka kwa Wataliban kwa kibali cha rais wa Afghanistan, Hamid Karzai. Lakini Wataliban hawana mpango wowote wa kusitisha mapigano na wananunua silaha zaidi Pakistan. (Afghanistan, "toonpool")
Ndiyo, anaweza
Hata katika nchi zilizo mbali na Ulaya inafahamika kwamba Angela Merkel ni kansela mkakamavu anayeendelea kuiongoza nchi yake ipate mafanikio. Nchini Marekani, ambapo hali ya kiuchumi si nzuri, watu wote, akiwemo rais Barack Obama, wanajiuliza Merkel anawezaje kuimarisha hali nchini mwake wakati Ulaya nzima iko katika mgogoro. (Marekani, "The Hartford Courant")
Ujuzi wa diplomasia
Katika siasa za kimataifa mwanasiasa haruhusiwi kusema wazi kile wanachokifikiria juu ya mwanasiasa mwenzake kutoka nje. Warusi wengi huenda wanamfananisha rais wao, Vladimir Putin na Angela Merkel. Hata hivyo, Merkel ana ushawishi mdogo tu katika nchi ya Putin. Licha ya hayo, Warusi wengi wamemkosoa yeye na wanasiasa wengine wa Ulaya kwa sababu hawamwekei Putin shinikizo. (Urusi, "facebook")
Bibi Merkel anasafiri
Hali inayofananishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe inaendelea Misri sasa. Lakini huko hakuna anayemuwaza Merkel. Katika nchi hiyo inayotawaliwa na wanaume kwa sehemu kubwa watu wanajiuliza inakuwaje Ujerumani itawaliwe na mwanamke. Akiwa mwakilishi wa taifa kubwa la kiuchumi barani Ulaya, Merkel anawakilisha pia bidhaa ya muhimu zaidi ya Ujerumani: "Magari kutoka Ujerumani." (Misri, "facebook")
Mgombea anayesumbua
Tabia ya Merkel ya kutafakari inawapendeza wananchi wengi. Wananchi wameweka imani yao kwa Merkel katika masuala yote. Chama chake kinakosolewa kwa mgogoro wa sarafu ya Euro na kashfa ya ndege zisizo na rubani, lakini hakuna anayemkosoa Merkel mwenyewe. Mgombea Peer Steinbrück wa SPD ana wakati mgumu. Hakuna anayemtambua kweli kama mpinzani wa Merkel. (Ujerumani, "Main-Post")