1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachambuzi waonya Al Shabab yatanua operesheni zake Kenya

Admin.WagnerD3 Juni 2015

Wapiganaji wa kundi la Somalia la Al Shabab wanazidi kutanua mashambulizi yao kaskazini mashariki mwa Kenya na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaitaka Kenya kuchukua hatua madhubuti kuwakata makali waasi hao

https://p.dw.com/p/1Fb3c
Picha: picture-alliance/dpa/ S. Y. Warsame

Kenya imeweza kuyatuma majeshi yake kwa wingi kusini mwa Somalia lakini inaonekana kushindwa kuyalinda maeneo kadhaa nchini mwake dhidi ya kitisho cha kundi la waasi la Al Shabab.

Maafisa wa usalama kutoka nchi za magaharibi wanaonya Kenya inapaswa kuchua hatua za haraka kulizuia kundi hilo dhidi ya kukita mizizi nchini humo na kuendelea kuwasajili vijana kuwa wapiganaji wake wapya.

Wachambuzi wanasema Al Shabab haina tena hamu ya kuendelea na operesheni zake Somalia kwani wameshindwa kutokana na kampeini kabambe ya kijeshi ya Umoja wa Afrika, wamepoteza makali na mashambulizi yao ambayo siku hizi si mengi kama miaka ya nyuma nchini Somalia, hayapati kuangaziwa pakubwa na vyombo vya habari.

Al Shabab wameelekeza uasi Kenya

Hali nchini Kenya ni tofauti, waasi hao wa Al shabab wamepata mazingira mapya ya kuendeleza itikadi zao za kijihadi, kupata wapiganaji wapya na uwezekano mkubwa wa kuiyumbisha nchi hiyo.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Makamu wa Rais William Ruto
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Makamu wa Rais William RutoPicha: AFP/Getty Images/S. Maina

Kenya imejikuta inakabiliwa na kibarua kigumu kufuatia kuibuka kwa seli za al shabab na mkakati wao wa kuyatuma majeshi yake mwaka 2011 kusini mwa Somalia kwa lengo la kulitokomeza kundi hilo na kuimarisha usalama katika mipaka yake kunaonekana kutozaa matunda yaliyohitajika.

Matokeo yake, waasi hao wamekuwa wakiingia na kutoka Kenya, wakifanya mashambulizi chungu nzima yakiwemo mauaji ya watu wengi na kurejea nchini mwao bila taabu licha ya mapambano makali kutoka kwa majeshi ya umoja wa Afrika na mashambulizi ya angani yanayofanywa na ndege za kijeshi zisioendeshwa na marubani za Marekani nchini Somalia.

Katika kaunti ya Mandera, abiria 28 waliokuwa wakisafiri kwa basi kutoka mji huo kuelekea Nairobi waliuawa na waasi hao mwaka jana, siku chache baadaye wafanyakazi wa mgodini 36 walishambuliwa na kuuawa katika eneo hilo hilo.

Mwezi Aprili mwaka huu, al shabab ilishambulia chuo kikuu cha Garissa na kuwaua takriban wanafunzi 150. Duru za kiusalama zinasesma waasi hao wa Al shabab wanafanya pia operesheni nyingine ambazo hazigongi vichwa vya habari kwasababu hakuna mauaji ya watu wengi lakini ambazo vile vile zinatia wasiwasi mkubwa.

Kwa mfano mwezi uliopita waasi hao waliingia katika kijiji cha Yumbis katika kaunti ya Garissa, kufanya ibada katika msikiti mmoja kwa saa kadhaa, kuwatisha wakaazi wa eneo hilo na kuondoka bila ya kupata pingamizi lolote.

Al Shabab yaingia na kutoka Kenya bila taabu

Wiki hii inaripotiwa waasi hao wameingia katika kijiji kimoja katika kaunti jirani ya Mandera na kusababisha shule kufungwa na wakaazi kuyatoroka makaazi yao.

Ramani ya Kenya ikionyesha maeneo ya ksakazini yanayoshambuliwa na Al Shabab
Ramani ya Kenya ikionyesha maeneo ya ksakazini yanayoshambuliwa na Al Shabab

Wataalamu wa masuala ya kiusalama wanaishauri serikali ya Kenya kuimarisha udhibiti wao katika maeneo ya mipaka ikizingatiwa kuwa vyanzo vingi mipakani havina ulinzi wa kutosha na hakuna miundo mbinu ya kuzuia kuingia na kutoka kwa urahisi kwa waasi hao.

Suala la iwapo Kenya inahitaji kuyaondoa majeshi yake nchini Somalia, limekuwa likizua mjadala mkali miongoni mwa wanasiasa nchini humo lakini inaonekana serikali ambayo imekuwa ikisisitiza haitayaondoa majeshi yake kwani kwa kufanya hivo ni kuwapa magaidi ushindi, inabadili mkakati.

Mwenyekiti wa kamati ya Seneti kuhusu usalama wa kitaifa na uhusiano wa nchi za kigeni Yusuf Hajji amedokeza katika mahojiano na kituo cha redio cha Kenya cha Capital kuwa mkakati wa kuyaondoa majeshi Somalia sio mwiko na ni jambo amablo linajadiliwa kwa kina kuona namna bora ya kulitekeleza na kuwahamisisha vijana kutoshawishika na itikadi kali za kijihadi kama sehemu ya kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo la Al Shabab.

Mwandishi:Caro Robi/afp

Mhariri: Yusuf Saumu