1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachambuzi: Bado kuna utata mkataba wa bandari Tanzania

23 Oktoba 2023

Baada ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai kusaini mikataba kuhusu uendeshwaji wa bandari ya Dar es salaam, wachambuzi wanansema bado kuna utata katika ubia huo, uliozua upinzani mkubwa ndani ya nchi.

https://p.dw.com/p/4Xts9
Bandari ya Dar es salaam-Tanzania
Bandari ya Dar es salaam-TanzaniaPicha: Xinhua/picture alliance

Baada ya miezi kadhaa ya wanaharakati, wanasiasa na baadhi ya viongozi wa dini kupinga mkataba kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai, kuhusu uwekezaji na uendeshaji wa bandari za Tanzania, jana Rais Samia Suluhu Hassan alisimamia utiwaji saini wa mikataba mitatu ya utekelezwaji wa makubaliano hayo kwenye Ikulu ya Chamwino, makao ya nchi, Dodoma.

Hatua hiyo imefanyika ikiwa bado kuna vuguvugu la upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati na wanasiasa wanaodai mkataba huo hauna faida kwa Tanzania.

Hebron Mwakagenda mmoja wa wanaharakati na wachambuzi wa siasa  Dar es Salaam anasema bado kuna utata anaouona katika ubia huo.

"Wasemaji wengi akiwemo rais, hawajaeleza faida tutazopata kwenye mkataba," Mwakagenda aliiambia Dw.

Soma pia:Tanzania: Wakosoaji wa mkataba wa bandari waachiliwe mara moja na bila masharti

Aliongeza kwamba kikubwa watanzania wanachotaka kusikia ni namna ambavyo mkataba huo utaongeza mapato ya nchi na ndani ya kipindi gani mafanikioa yataanza kuonekana.

Miongoni mwa vipengele vilivyoainishwa katika mkataba huo ni pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari ya Tanzaia, TPA, kuweza kuamua kuhamia kwenye kampuni ya DP World, na kwamba ingawa mkataba huo ni wa miaka 30, lakini utakuwa ukifanyiwa tathmini kila baada ya miaka mitano.

Hata hivyo, hili la tathmini kila baada ya miaka mitano, limezuwa maswali kadhaa ya kisheria na utekelezaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Bob Chacha Wangwe anasema mikataba mitatu iliosainiwa hapo jana Jumapili hairekebishi kile ambacho watanzania walikipinga tangu awali.

"Rais anasema maoni yalifanyiwa kazi, ni vizuri mikata iwekwe hadharani." Alisema Wangwe ambae pia kitaaluma ni mtaalamu wa sheria.

Wananchi wanahitaji elimu kuhusu mkataba

Jijini Dar es Salaam ndipo ilipo bandari kuu na ambayo ndiyo hasa iliyozuwa malumbano makali kuhusiana na mkataba huu.

Baadhi ya wakaazi ambao wengine wamehoji muendelezo wa ushirikiano huu wanasema hoja ya muda wa utekelezwaji wa mkataba ni vipi serikali imeshughulikia.

Baadhi ya wananchi wakiwa kando na Bandari ya Dar es salaam wakiangalia meli ya mizigo
Baadhi ya wananchi wakiwa kando na Bandari ya Dar es salaam wakiangalia meli ya mizigoPicha: Daniel Hayduk/AFP via Getty Images

Shadida Dalanga mkaazi wa Dar es salaam anasema elimu katika ubia ambao selikali imeingia na kampuni hiyo ya kimataifa ni jambo muhimu ili kufuta sintofahamu zinazojitokeza mara kwa mara.

Soma pia:Spika azuia mjadala kuhusu mkataba wa bandari ya Tanzania

"Tumesikia serikali imesaini mkataba wa miaka mia moja, hebu tuelimishwe hukusu hili." aliiambia DW.

 Licha ya ukosoaji huo, kwenye utiwaji saini mikataba hiyo hapo jana ilifahamika kuwa kinyume na madai ya awali, serikali ya Tanzania inayo haki ya kujiondoa, sheria za Tanzania zitatumika katika uendeshaji wa mkataba wenyewe, wazawa watakuwa na fursa za kuwekeza na kwamba mwekezaji -  ambaye ni DP World - atakuwa na wajibu wa kulipa tozo na kodi zote kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

DP World itaendesha magati manne ya bandari

Serikali ya Tanzania ilitia saini mkataba wenye utata wa usimamizi wa bandari na kampuni ya DP World yenye makao yake Dubai, ambao ulichochea maandamano katika nchi hiyo ya Afrika katika miezi iliyopita na kusababisha kukamatwa kwa wakosoaji kadhaa.

Mkataba huo ulitiwa saini jana Jumapili mbele ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Plasduce Mbossa alisema kuwa kampuni ya DP World yenye makao yake makuu katika Umoja wa Falme za Kiarabu, itaendesha magati manne pekee ya Bandari ya Dar es Salaam, iliyo katika mtaji wa kifedha wa nchi, na si bandari nzima.

Utendaji wake ungekaguliwa kila baada ya miaka mitano kwa kipindi cha jumla cha miaka 30 cha mkataba.

Upinzani na mashirika ya kiraia wameipinga serikali kuamua kuwa na kampuni ya kigeni inayosimamia bandari za Tanzania.

Hata hivyo serikali imesema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa bandari na kukuza uchumi wa nchi.

Kutana na mwanamke mwendesha mitambo bandarini Mtwara

Soma pia:Kanisa la KKKT launga mkono mkataba wa DP World ya Dubai.

Mkataba huo wa bandari uliidhinishwa na bunge la Tanzania Juni 10, na kusababisha maandamano ambapo zaidi ya watu 22 walikamatwa, kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.

Mwezi Agosti shirika hilo liliitaka Tanzania kuheshimu uhuru wa kujieleza na haki ya kuandamana.

Tanzania imefanya mageuzi kadhaa tangu kifo cha Rais Magufuli mwaka 2021, ambaye aliwakandamiza wakosoaji na kuanzisha sheria kali.