1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Ujerumani waipitisha bajeti

Abdu Said Mtullya19 Machi 2010

Wabunge wa Ujerumani leo wameipitisha bajeti ya waziri wa fedha Wolfgang Schäuble.

https://p.dw.com/p/MXpG
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: AP

Wabunge wa Ujerumani leo wameipitisha bajeti ya mwaka huu wa fedha,jumla ya Euro Bilioni 320,lakini wajumbe wa vyama vya upinzani wameilaumu serikali kwa kukusudia kuongeza denila nchi hadi Euro bilioni 82.

Waziri wa fedha wa Ujerumani,Wolfgang Schäuble,leo amesisitiza ulazima wa kurejea katika njia ya matumizi bora ya fedha ili kukabiliana na deni hilo.

Akizungumza bungeni,kuchangia katika mjadala wa bajeti ya Ujerumani kwa mwaka mpya wa fedha, waziri Schäuble ametangaza mpango kabambe utakaowezesha kuziweka sawa hesabu za fedha mnamo miaka inayofuata .

Waziri huyo amesema lazima Ujerumani irejee katika njia ya matumizi bora ya fedha ili kuweza kuziweka sawa hesabu za nchi.

Wabunge wa Ujerumani wameipitisha bajeti hiyo ya Euro Bilioni 320, lakini serikali inatarajiwa kuongeza deni kwa Euro Bilioni 82. Kiwango hicho hakijawahi kufikiwa katika historia ya Ujerumani.

Hata hivyo,waziri wa fedha Schäuble amesema bidii kubwa zitafanywa ili kulipunguza deni hilo hatua kwa hatua .

Katika bajeti ya mwaka huu,kiasi cha Euro Bilioni 319 kitatengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mapato ya yanatarajiwa kufikia kiasi cha Euro Bilioni 211.

Serikali pia itatenga kiasi cha Euro Bilioni 28 kwa ajili ya kuekeza katika vitega uchumi. Wabunge wa vyama vya upinzani wameilamu serikali kwa mpango wa kuongeza deni

Hapo awali,kiongozi wa wabunge wa chama cha SDP, Frank- Walter Steinmeier,amesema walipa kodi sasa watalipa kwa niaba ya mawakala wa ulanguzi na mabenki yenye uchu wa faida.

Wabunge 313 walipiga kura kuipitisha bajeti hiyo na 256 waliipinga.

Mwandishi Mtullya Abdu/DPA/ZA

Mhariri: Miraji Othman