1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa NRM wampinga Museveni hadharani

24 Oktoba 2011

Hali ya mvutano imeibuka ndani ya chama tawala cha NRM nchini Uganda kuhusu kandarasi za uchimbaji wa mafuta nchini Uganda, huku wabunge wa chama hicho wakiunga mkono msimamo wa Bunge na wakikaidi mapendekezo ya Rais.

https://p.dw.com/p/12y1h
Rais Yoweri Museveni wa Uganda
Rais Yoweri Museveni wa UgandaPicha: DW/Schlindwein

Ni pendekezo ambalo halikuungwa mkono na baadhi ya wabunge wa NRM. Lakini baada ya kuujadili msimamo wa bunge kwa kusitisha mipango yote ya serikali kutoa kandarasi kwa kampuni ya Ufaransa ya Total na ile ya China ya CNOOC, Museveni alishikilia msimamo wake kuwa uamuzi wa bunge unafaa kupinduliwa ili serikali isipoteze takriban dola za Kimarekani bilioni tatu, kupitia mkataba wa kuziruhusu Total na CNOOC kuchimba mafuta.

Msimamo wa Rais Museveni uliwakasirisha baadhi ya wabunge wa chama chake na kilichofuatia ni wabunge saba kuondoka kwenye kikao hicho.

Miongoni mwa walioondoka ni mbunge Theodore Sekikubo, ambaye anasema kwamba walitoka nje ya kikao "kuonyesha kutoridhika kwetu na vile nguvu za bunge zilikuwa zinadharauliwa na chama".

Pendekezo jengine kutoka kwa rais ni mawaziri watatu ambao wanasemekana walipokea rushwa kutoka kwa kampuni ya mafuta ya Uingereza ya Tullow kutojiuzulu wakati uchunguzi ukiendelea ingawa bunge lilikuwa limeamua wajiuzulu.

Wapinzani nchini Uganda wakiandamana dhidi ya Rais Museveni.
Wapinzani nchini Uganda wakiandamana dhidi ya Rais Museveni.Picha: dapd

Mawaziri hawa ni waziri mkuu Amama Mbabazi, waziri wa nje, Sam Kutesa, na waziri wa mambo ya ndani, Hillary Onek, ambaye wakati hongo hizi zikitolewa alikuwa waziri wa nishati.

Mbunge mwingine ambaye aliupinga uamuzi wa Museveni anasema Museveni anawatetea mawaziri hawa kwa sababu anahisi kuwa sura ya serikali yake itaharibika vibaya sana kwa sababu ataonekana kama kiongozi anayewateuwa watu walio wafisadi. "Ikiwa hatawaambia waondoke kwa hiyari yao, basi tutakachofanya ni kuwachunguza na tukigundua walipokea rushwa, tutawatupa nje ya bunge".

Rais Museveni ametishia kuwafukuza kutoka chama chake wabunge wa chama hicho ambao wanakiuka maadili ya chama tawala. Akiyazungumzia matamshi ya Museveni Mbunge Wilfred Niwagaba alisema ilimradi tu kumfukuza kutoka hakutamaanisha kumfukuza kutoka Uganda, "anaweza kufanya atakacho".

Mbunge Barnabas Tinkasimire akiuzungumzia utawala wa Museveni alisema, kiongozi akikaa mamlakani kwa kipindi kirefu anaanza kutumbayumba. "Raia wa Uganda hawatarajii rais Museveni kufanya uamuzi kama huu na anawasaliti raia wake. Nadhani wakati umefika wa Rais Museveni kusema hawezi kulistahimili shinikizo anayoipata na ni heri kumwachia mtu mwingine aendelee na uongozi".

Msemaji wa serikali, Mary Karooro Okurut, amesema hawezi kulizungumzia suala hili na kuitaka Deutsche Welle izungumze na mwenyekiti wa NRM Bungeni, David Bahati, ambaye hakuweza kupatikana kwa simu kwa sababu alikuwa ikulu akikutana na Rais Museveni.

Hii ndio mara ya kwanza ya Rais Museveni kupata upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa chama chake mwenyewe.

Ripoti: Leylah Ndinda, Kampala. Mhariri: Josephat Charo