Wabunge wa Marekani wamkosoa Trump namna alivyoitetea Urusi
17 Julai 2018Akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya uchunguzi dhidi ya Urusi, Trump amesema hapakuwa na njama ya aina yoyote na kwamba ametumia muda mwingi kuzungumza na rais wa Urusi Vladmir Putin kuhusu madai hayo ya kuingilia uchaguzi. Trump amesema ana imani na idara za upelelezi za Marekani, lakini akadokeza kwamba Putin alikuwa mwenye nguvu kuyakataa madai hayo, na kisha alimsifu rais huyo wa Urusi kwa kuahidi kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi unaoendelea.
Ameuita uchunguzi huo maalum kuwa janga na kudai kwamba timu yake ya kampeni ilifanya kazi nzuri na ndio sababu alichaguliwa kama rais. "Ninachoweza kufanya ni kuuliza. Watu wangu walinijia, Dan Coats alikuja kwangu na wengine wakisema wanadhani ni Urusi. Niko na rais Putin na amethibitisha haikuwa Urusi, kwahiyo naweza sema sioni sababu kwanini wawe wao," alisema Trump.
Baada ya Trump kutoa kauli hiyo, maafisa wa upelelezi na viongozi waandamizi wa chama cha Republican walimkosoa Trump kama kiogozi wa "aibu” na "asiye na heshima” baada ya kushindwa kumkabili rais wa Urusi Vladmir Putin juu ya madai ya kuingilia uchaguzi wa 2016.
Seneta wa Republican John McCain alisema Trump kukubali utetezi wa Putin juu ya madai hayo ni kitendo cha kujishusha kwa rais wa Marekani na kwamba mkutano huo wa Helsinki ulikuwa "kosa baya”.
"Mkutano wa waandishi wa habari huko Helsinki ulikuwa moja ya mikutano ya aibu zaidi katika kumbukumbu ya historia ya marais. Uharibifu unaosababishwa na ukosefu wa busara, kujikuza, uwiano wa uwongo, na huruma yake kwa marais madikteta ni vigumu kuuhesabu”, alisema McCain katika taarifa yake.
Akizungumzia suala hilo moja kwa moja na rais aliyemteua, mkurugenzi wa usalama wa taifa Dan Coats alisema mashirika ya kipelelezi ya Marekani yamekuwa "wazi” na "hoja za kweli” katika tathmini yake kwamba Moscow iliingilia uchaguzi wa rais miaka miwili iliyopita, tathmini ambayo Trump amekataa kuiunga mkono mjini Helsinki. Coats anasema Urusi bado inaendelea na jitihada za kutaka kudhoofisha demokrasia ya Marekani.
Kauli za Trump za kuitetea Urusi zinatolewa siku tatu baada ya wizara ya sheria ya Marekani kubainisha maafisa 12 wa Urusi kwamba walidukua kompyuta za chama cha Democratic, ikiwa ni hatua za karibuni kuchukuliwa na serikali ya Marekani tangu mwishoni mwa mwaka 2016 katika kile idara za usalama za Marekani zinakielezea kwamba ulikuwa ni mpango mpana wa kusadia kampeni za Trump ulioelekezwa na Putin mwenyewe.
Lakini bado Trump alionekana kuyaamini maneno ya Putin na kutupilia mbali taarifa hizo. Spika wa bunge la wawakilishi Paul Ryan alisema Trump "ni lazima atambue kwamba Urusi sio mshirika wetu. Hakuna uwiano wa kiimaadili baina ya Marekani na Urusi ambayo bado inadharau misingi yetu na mawazo”.
Seneta Lindsey Graham alisema majibu ya Trump kuhusu madai ya kuingiliwa kwa uchaguzi yatachukuliwa na Urusi kama ishara ya udhaifu. Naye seneta wa Arizona Jeff Flake aliandika, "ni aibu, sijawahi kufikiria kama siku moja nitashuhudia rais wa Marekani amesimama jukwaani na rais wa Urusi na kutupa lawama zote kwa Marekani juu ya uchokozi unaofanywa na Urusi”.
Adam Schiff, seneta mwandamizi wa Democratic katika kamati ya bunge ya usalama alisema Trump amempatia taa nyekundu Putin ya kuingilia tena uchaguzi huo mwaka 2018.
Viongozi hao walikuwa na mazungumzo mjini Helsinki Finland kama njia ya kuimarisha mahusiano ya nchi hizo na kudai kwamba majadiliano ya kina yalikuwa ni muhimu kwa nchi zote mbili.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga