Wabunge wa Marekani wakubaliana muswada wa sheria ya bunduki
22 Juni 2022Wabunge hao kutoka vyama vyote viwili vya Republican na Democrat wameelezea imani yao kwamba sheria hiyo itapitishwa na itasaidia pakubwa kudhibiti umiliki wa bunduki na hatimaye kukabiliana na ogezeko la matukio ya mashambulizi ya bunduki yanayoibua hofu kubwa nchini Marekani.
Wabunge hao amesema wana uhakika kwamba sheria hiyo itaungwa mkono na pande zote mbili na huenda ikamfikia rais Joe Biden wiki ijayo.
Kiongozi wa maseneta wa chama cha Democrat Chuck Schumer amenukuliwa akisema sheria hiyo ya usalama wa bunduki ni hatua kubwa na itasaidia kuokoa maisha. Amesema ingawa haijajumuisha kila kiu wanachokihitaji, lakini inahitajika kwa dharura.
Kundi hilo la wabunge lilikubaliana kuhusu mfumo ambao utajumuisha uchunguzi wa kina historia ya wanunuzi walio na umri wa chini ya miaka 21 na ufadhili wa afya ya akili pamoja na programu za usalama shuleni. Muswada huo pia unatoa mwito wa ufadhili ili kuyawezesha majimbo kutekeleza sheria ya kuzichukua silaha kutoka kwa watu wanaodhaniwa kuwa kitisho.
Hatua hizo zinataraji kugharimu karibu dola bilioni 15 ambazo seneta Chris Murphy wa Connecticut na kiongozi wa wabunge wa Democrat kwenye kundi hilo, amesema zitatolewa.
Wabunge wasisitiza wanataka kufanya kitu cha msingi.
Hata hivyo wabunge hao wamechelewa kuwasilisha muswada huo wenye kurasa 80, licha ya kutambua kwamba kuchelewa huko kunaondoa maana ya udharura uliochochewa na shambulizi la bunduki kwenye shule ya msingi ya Robb katika jimbo la Texas na kusababisha vifo vya watoto 19 na walimu wawili na menginyeyo yaliyotokea katika miezi ya karibuni.
Seneta wa jimbo la Texas John Cornyn amesema anataka kuhakikisha kwamba wanafanya ktiu cha msingi kitakachoweza kukubalika na kuwa sheria na kunusuru maisha ya wengi.
Amesema "Mheshimiwa Rais, siku 28 zilizopita, kijana wa miaka 18 aliwafyatulia risasi wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Robb huko Uvalde, Texas. Aliua watu 21, watoto 19 na walimu wawili. Hili lilikuwa ni shambulio la kikatili. Nimepokea simu na barua pepe nyingi zenye ujumbe mmoja, kwamba "Fanya jambo." Fanya kitu." Wana-Texas wamekerwa na kilichotokea katika Shule ya Msingi ya Robb, na wanataka bunge kuchukua hatua zinazofaa. Nataka kuhakikisha kweli tunafanya kitu chenye manufaa kitu ambacho kina uwezo wa kuwa sheria na kuokoa maisha."
Sheria muhimu ya shirikisho iliyohusiana na udhibiti wa bunduki ilipitishwa mara ya mwisho mwaka 1994. Ilizuia utengenezaji wa bunduki za maangamizi zinazoweza kutumiwa na raia na zenye uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya risasi. Hata hivyo sheria hiyo ilifikia ukomo wake miaka kumi baadae na tangu hapo hakukua na juhudi zozote za maana za kufanya maboresho licha ya wastani wa ongezeko la kila siku la mauaji ya watu wengi kuongezeka hadi 11 mwaka huu, hii ikiwa ni kulingana na ofisi inayohifadhi taarifa za visa vya uhalifu wa bunduki.
Hata hivyo Chama cha Kitaifa cha Bunduki kimeyapinga mapendekezo hayo kikisema yana mapungufu katika kila eneo. Kimesema yanaonyesha yatasaidia kidogo kushughulikia uhalifu huo.
Muswada huo utahitaji kura za angalau wabunge 10 wa Republican ili kufikia 60 ambazo huhitajika wakati sheria muhimu zinapopitishwa, ingawa sintofahamu inasalia kuhusiana na iwapo makubaliano hayo ni mwanzo mpya wa hatua za bunge za kudhibiti uhalifu wa bunduki.
Mashirika: AFPE/APE