1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa democratic wamchunguza Trump upya

5 Machi 2019

Wabunge wa chama cha democratic nchini Marekani wameanzisha uchunguzi mpya dhidi ya Rais Donald Trump, ambao unatishia kumzonga rais huyo hadi msimu wa uchaguzi wa mwaka 2020.

https://p.dw.com/p/3ERne
Präsident Trump umarmt die US Flagge
Picha: picture-alliance/Katopodis

Uchunguzi huo unahusisha shughuli za ikulu ya White House, kampeni, na biashara za familia yake.

Mwenyekiti wa kamati ya sheria ya bunge la Marekani Jerrold Nadler amesema jopo lake linaanza uchunguzi kuhusu uwezekano wa kuzuia haki, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka na ameitisha nyaraka kutoka kwa watu 81 wanaohusishwa na Rais Trump na washirika wake. Jamie Raskin ni mwanachama wa kamati hiyo.

Huenda uchunguzi huo ukatoa nafasi ya juhudi za kumuondoa madarakani Trump

"Kamati ya sheria ya bunge imetuma maombi ya stakabadhi kwa watu 81 ambao wana taarifa zinazohusiana na uchunguzi wetu wa matumizi mabaya wa mamlaka na uhalifu mwengine ambao unaweza kuwa umefanyika katika ikulu ya White House. Kwa hiyo kila mmoja ya hawa watu wametumiwa maombi binafs ya stakabadhi," alisema Raskin.

USA Washinton DC - Kongressmitglieder vor dem Capitol Hill
Wademocrat walichukua udhibiti wa bunge na wameanza kumpa shinikizo TrumpPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Uchunguzi huo mpana huenda ukawa unatoa nafasi kwa juhudi za kumuondoa madarakani Trump ingawa viongozi wa chama cha Democratic wameapa kuwa wataangazia njia zote na kuitathmini ripoti ya wakili maalum Robert Mueller kabla kuchukua hatua yoyote ile. Wademocrat walichukua udhibiti wa Bunge la Wawakilishi na tayari wameanza kutumia mamlaka yao kumuwekea shinikizo rais.

Trump amezungumza na wanahabari baada ya tangazo la uchunguzi huo na kusema atashirikiana na wanaofanya uchunguzi huo.

"Kila wakati nashirikiana na kila mmoja. Unajua, uzuri ni kwamba yote haya ni uongo mtupu," alisema Trump.

Majina ya watu waliotajwa ni 81 na yanahusish maisha ya Rais Trump

Msemaji wa ikulu ya Marekani Sarah Sanders amedai kuwa uchunguzi huo ni wa aibu na kudhalilisha kuhusiana na mambo ya uongo. Amedai kuwa Nadler na Wademocrat wenzake wameanzisha uchunguzi huo wa uongo kutokana na kuwa wana hofu kwamba jambo ambalo wamekuwa wakilisema kwa miaka miwili la Trump kushirikiana na Urusi kushinda uchaguzi, kwa sasa linaanza kukosa mashiko.

Sarah Sanders Trump PK Sprecherin
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sarah SandersPicha: picture-alliance/dpa/M. Brochstein

Majina hayo 81 yaliyoko kwenye orodha ya kamati hiyo ya bunge yote yanagusia maisha ya Trump  kuanzia ikulu, biashara, kampeni yake na kamati iliyosimamia kipindi cha mpito kutoka kampeni hadi urais. 

Kamati hiyo pia inalitaka shirika la upelelezi la Marekani FBI, Idara ya Haki na idara zengine kuwasilisha stakabadhi zinazohusiana na kuachiwa kwa wakili wa zamani wa Trump Mchael Cohen, mshauri wa usalama wa kitafa wa zamani Michael Flynn na mwenyekiti wa zamani wa kampeni ya Trump Paul Manafort.