Wabunge Marsabit wataka operesheni dhidi ya bunduki haramu
25 Juni 2020Wabunge hao wanashikilia kuwa, mauaji ambayo yamekuwa yakiripotiwa kila mara ni ishara kwamba, silaha zingali mikononi mwa raia licha ya operesheni ya kijeshi mwaka uliopita.
Katika kipindi cha mwezi mmoja sasa, watu zaidi ya ishirini wameuawa kwa kupigwa risasi katika maeneo tofauti ya jimbo hilo katika kile kinachoaminika kuwa ni mzozo wa kikabila Marsabit.
Visa vya mauaji hayo sasa vimewachochea wabunge wanawake katika bunge la kaunti, kuitaka wizara ya usalama kuanzisha operesheni kali ya kusaka bunduki haramu zilizoko mikononi mwa raia pamoja na kuwakamata wanaofanya mauaji hayo.
Idara ya uendesha mashtaka yakosolewa
Katika mkutano na waandishi wa habari katika majengo ya bunge la kaunti, wabunge hao wameikosoa idara ya uendeshamashtaka kwa kushindwa kuwakamata wanaowaua raia bila hatia yoyote.
"Tunauliza kama akina mama,kazi ya NIS na DCI hapa Marsabit ni nini kwa sababu Watoto wetu bila hatia wanauawa kila wakati.Tunaendelea kuwazika mmoja baada ya mwingine.Vikundi vingi kama UNDP wamejaribu kuongea juu ya amani lakini bado” Amesema Asunta Galgidele ambaye ni mbunge wa wadi ya Korr/Kargi kwenye bunge la kaunti hiyo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya usalama katika bunge la kaunti hiyo Kiya Jillo, wakati umewadia kwa wizara ya usalama kuokoa maisha ya wakaazi wa Marsabit kwa kuendesha operesheni kali ya kijeshi ya kusaka bunduki na silaha nyingine zinatotumika kuwaua raia. Ameendelea kusema kuwa: "Ninayoomba zaidi ni kwa ofisi ya waziri matiangi walete operesheni kali kabisa hapa marsabit ili silaha haramu zichukuliwe zote”
Waziri wa ndani Fred Matiangi atangaza msako dhidi ya wachochezi
Mwaka jana, serikali ilianzisha operesheni ya kijeshi Marsabit kusaka silaha haramu baada ya mauaji ya watu kumi na watatu eneo la Qubi Qallo na idara ya usalama ilitangaza kufaulu kwenye operesheni hiyo.
Wiki mbili zilizopita, waziri wa usalama wa ndani Dakta Fred Matiangi alitangaza kuwa wizara yake itawakamata wanasiasa wachochezi kutoka Marsabit katika hatua ya kumaliza vita hivyo vya kikabila.
"Wakati maneneo haya yanapotekea,baadhi wanacheza siasa na wanakwepa mkono wa sheria na kisha baadaye wanaendelea kuwachochea wananchi. Wanadhani njia bora ya kupata uungwajimkono ni kuwawezesha jamii moja kupata silaha” Amesema Dr. Matiangi.
Idadi kubwa ya waliofariki tangu machafuko ya kikabila kuzuka Marsabit ni wanafunzi na wizara ya usalama inaendelea na uchunguzi wake kuwakamata waliohusika.
Kufikia sasa, watu wanne wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Laisamis wakihusishwa na mauji hayo wakiwemo baadhi ya wanasiasa