1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabosnia waadhimisha miaka 25 ya mauaji ya Srebrenica

11 Julai 2020

Wabosnia Jumamosi wamefanya kumbukumbu ya mauaji ya Waislamu 8,000 huko Srebrenica hiyo ikiwa miaka 25 tangu kufanyika kwa mauaji hayo ambayo yamekuwa udhalimu mkubwa kufanyika Ulaya tangu Vita vya Pili Vikuu vya Dunia.

https://p.dw.com/p/3fAAX
Bosnien und Herzegowina Gedenken an Srebrenica-Massaker
Picha: Getty Images/D. Sagolj

Familia zinazoomboleza zilisimama mbele ya majeneza tisa ya wahanga wapya waliotambuliwa yaliyokuwa yamefunikwa kwa kitambaa cha kijani. Wahanga hao wapya watazikwa katika eneo la makaburi lililo na umbo la ua sehemu iliyo na makaburi ya wahanga wengine 6,643. Karibu wahanga 1,000 wa mauaji hayo ya halaiki katika mji huo wa mashariki yaliyotokea wakati wa vita vya Bosnia vya kati ya mwaka 1992-1995 bado hawajulikani walipo.

Viongozi wa dunia wamehutubia sherehe hizo za maadhimisho kwa njia ya video kwani hawakuweza kuhudhuria kutokana na janga la virusi vya corona. Makumi kwa maelfu ya watu huhudhuria maadhimisho hayo kila mwaka ila safari hii waandalizi waliwakubalia watu wachache tu.

Kamanda Ratko Mladic aliwaongoza wanajeshi wa Serbia kuivamia Srebrenica

Wakati wa vita vya Bosnia, wanajeshi Waserbia wa Bosnia waliwafukuza watu ambao si raia wa Serbia kutoka maeneo hayo. Waislamu waliokuwa wanatoroka walijificha katika miji ya mashariki ukiwemo mji wa Srebrenica ambao ulikuwa ni mmoja wa miji iliyokuwa imedaiwa kuwa maeneo salama yaliyotengwa na Umoja wa Mataifa.

Bosnien und Herzegowina - Gedenken an Srebrenica-Massaker
Wanawake wakilia katika jeneza la mpendwa waoPicha: Reuters/D. Ruvic

Mnamo Julai 11, 1995 wanajeshi wa Serbia wakiongozwa na Kamanda mkuu Ratko Mladic waliwazidi nguvu wanajeshi wa Umoja wa Maztaifa na kuvamia mji wa Srebrenica uliokuwa unalindwa na kikosi cha kulinda amani cha Uholanzi kilichokuwa na silaha hafifu. Wanawake na watoto walitenganishwa na wanaume na wakapelekewa katika eneo linalodhibitiwa na jeshi la Bosnia.

Wanaume na wavulana waliuwawa na waliokuwa wakijaribu kutoroka kupitia misituni walikamatwa na kuuwawa. Miili yao ilizikwa katika makaburi ya halaiki ambayo baadae yalifukuliwa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa na kutumiwa kama ushahidi katika kesi za uhalifu wa kivita dhidi ya viongozi wa Bosnia na Serbia.

Wabosnia wengi ndio waliohudhuria maadhimisho hayo

"Tunaomboleza na familia ambazo zimekuwa zikitafuta haki bila kuchoka kwa miaka yote hii," alisema Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo katika hotuba yake. Marekani ndiyo iliyosimamia mkataba wa amani wa Bosnia miezi kadhaa baada ya mauaji hayo ya halaiki.

Bosnien und Herzegowina | Gedenken an Srebrenica-Massaker
Waombolezaji wakitazama hotuba za viongozi wa dunia kwa njia ya videoPicha: picture-alliance/AA/S. Jordamovic

Idadi kubwa ya waliohudhuria maadhimisho hayo walikuwa Wabosnia ambao ni Waislamu jambo linaloonyesha kwamba Bosnia haijafanikiwa kupata maridhiano miaka 25 tangu kukamilika kwa vita vyake ambapo karibu watu 100,000 waliuwawa.

Mahakama ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu wa kivita katika iliyokuwa Yugoslavia ilimhukumu Mladic pamoja na mkuu wake wa kisiasa Radovan Karadzic kutokana na mauaji ya halaiki ya Srebrenica ingawa wanasalia kuwa mashujaa kwa Waserbia ambao idadi kubwa wanakanusha kwamba kulitokea mauaji hayo ya halaiki.