1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabelgiji washinda kwa jasho dhidi ya Algeria

18 Juni 2014

Ubelgiji ilitokwa jasho kwa dakika 70 za mchezo dhidi ya safu ngumu ya ulinzi ya Algeria. Lakini wachezaji wawili wa akiba walioingia kama nguvu mpya waliipa Ubelgiji ushindi wa magoli mawili kwa moja.

https://p.dw.com/p/1CKqN
FIFA Fußball WM 2014 Algerien Belgien
Picha: Getty Images

Huku ikikabiliwa na mbinyo wa kupigiwa upatu na karibu kila mmoja kuwa timu inayotarajiwa kusababisha mshangao katika fainali hizi, Ubelgiji waliingia katika dimba lao la kwanza la Kombe la Dunia tangu mwaka wa 2002 wakionekana kama wanaoweza kuwa washindi.

Kikosi hicho cha kocha Marc Wilmots chenye vipaji kilitokwa jasho kuivunja ngome ya Algeria kwa kipindi kirefu cha mchezo, kwa kuonyesha mchezo usiovutia machoni na hasa katika kipindi cha kwanza.

FIFA Fußball WM 2014 Algerien Belgien
Algeria walitangulia kuwa kifua mbele kupitia mkwaju wa penalti uliofungwa na Sofiane FeghouliPicha: picture-alliance/AP

Algeria ilionekana kujituma, hasa kutoka kwa mshambuliaji wao Sofiane Feghouli. Feghouli alipata penaltio baada ya kuangushwa na beki wa Ubelgiji Jan Vertonghen katika dakika ya 20. Nyota huyo wa klabu ya Valencia alisukuma wavuni kombora safi ambalo mlinda lango wa Ubelgiji Thibaut Courtois alikosa maarifa ya kulizuia.

Licha ya kuutawala mchezo, Wabelgiji hawakuwa na jawabu lolote kabla ya kuamua kutafuta msaada kutoka kwenye benchi la wachezaji wa akiba. Dries Mertens aliingia uwanjani katika kipindi cha pili, pamoja na Marouane Fellaini. Hapo ndipo vijana wa Wilmots walipoongeza kasi na kuanza kuifungua safu ya ulinzi wa Algeria.

Nyota wa Wolfsburg Kevin de Bruyne, alipiga krosi safi ambayo iliunganishwa kwa njia ya kichwa na Fellaini hadi wavuni. Bao hilo la kusawazisha liliitikisha Algeria ambayo ilionekana kulegea kidogo na kuiruhusu Ubelgiji kuanza kuutawala mchezo na kushambulia. Muda mfupi baadaye, shambulizi la kasi lilifanyika baada ya de Bruyne kuupata mpira katikati ya uwanja na kutimka nao kabla ya kumsukumia Edin Hazard ambaye alimwandalia pasi safi Dries Mertens ambaye alivurumisha shuti kali jadi nyavuni na kuwapa Ubelgiji ushindi.

Ubelgiji hivyo basi wamepata pointi tatu kutokana na mechi yao ya kwanza ya makundi. Mbele ya Korea Kusini na Urusi ambazo zimetoka sare ya kufungana goli moja kwa moja.

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Abdul-Rahman