1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wauteka mji wa Bangassou Jamhuri ya Afrika ya Kati

Saleh Mwanamilongo
4 Januari 2021

Waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameuteka mji wa Bangassou, masharaki mwa mji mkuu Bangui, siku moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais na bunge ulioitishwa Desemba 27.

https://p.dw.com/p/3nUvN
Zentalafrikanische Republik UN Mission MINUSCA
Picha: picture-alliance/AA/H.C. Serefio

Mji wa Bangassou wenye utajiri wa madini ya almasi unapatikana umbali wa kilomita 750 na mji mkuu Bangui. Rosevel Pierre Louis, mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, MINUSCA, kwenye eneo hilo amesema kwamba waasi waliushambulia mji huo mapema siku ya Jumapili na waliushikilia kwa muda wa saa kadhaa baada ya mapambano makali.

Kikosi cha MINUSCA kilitangaza kwamba wapiganaji watano waliuawa, bila kutoa maelezo zaidi. Kwa upande wake shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF lilitangaza kwamba liliwahudumia watu zaidi ya kumi na watano waliojeruhiwa. Desemba 19, makundi ya waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, yalitangaza kuungana pamoja na kuanzisha mapigano ili kuudhibiti mji mkuu Bangui na kuvuruga maandalizi ya uchaguzi wa rais na bunge.

Lakini waasi hao hadi sasa wamezuiliwa kuuteka mji mkuu na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa taifa. Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanaungwa mkono na wale wa Rwanda na mamluki kutoka Urusi. Jumamosi waasi waliushambulia mji wa Damara, alikotoka rais wa sasa Faustin Archange Touadera, ulioko umbali wa Kilomita 70 kaskazini mwa Bangui. Duru zinaeleza kwamba waasi hao walirejeshwa nyuma na vikosi vya Umoja wa Mataifa.

Zentralafrikanische Flüchtlinge auf dem Weg zum Bus
Raia wakikimbia machafuko Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: Kouam Joel Honore

Roland Marchal, mtaalamu wa masuala ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenye kituo cha utafiti wa kimataifa mjini Paris, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba waasi hao waliamini kuuteka mji mkuu bila vipingamizi bila kujali ujio wa wanajeshi wa Urusi na Rwanda.

Nathalie Dukhan, mtaalamu wa Afrika ya Kati kwenye shirika la kimarekani The Sentry amesema kwamba waasi hao wana malengo ya muda mrefu ambayo kwanza ni kudhibiti miji yenye utajiri wa madani na itakayowawezesha kujimudu kwa silaha na vifaa vya kivita.

Kwenye hotuba yake mkesha wa mwaka mpya, Rais Touadera alisema nchi yake iko kwenye vita na kuahidi kwamba taifa hilo litapata ushindi dhidi vita hivyo.

Kutekwa kwa mji wa Bangassou, kumetokea siku moja kabla ya kutangazwa hii leo na tume ya taifa ya uchaguzi kwa matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais na bunge. Theluthi mbili ya ardhi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imedhibitiwa na makundi ya waasi. Na majimbo ya uchaguzi 29 miongoni mwa 71 hayakupiga kura wiki iliyopita, alisema Mamokoama Theophile, msemaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Zentralafrikanische Republik Präsident und Rebellen unterzeichnen Friedensabkommen in Bangui | Sidiki Abbas
Sidika Abbas kiongozi wa kundi la waasi huko Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: Getty Images/AFP/F. Vergnes

Maafisa wa Jeshi, kwenye jimbo la Sud-Ubangi kaskazini mwa Kongo wamesema machafuko ya hivi karibuni nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yamesababisha maelfu ya raia kuvuka mpaka na kuingia nchini Kongo. Na kusababisha wanajeshi kuwa katika hali ya tahadhari,kwa mujibu wa radio Okapi ya Umoja wa Mataifa.

Shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Kongo, limesema lilisitisha zoezi la kuwarejesha wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya kati waliokuwa wakiishi nchini Kongo.

Wakimbizi hao ambao walikimbia vita miaka mitatu iliopita walikuwa wakiishi kwenye miji ya Zongo na Libenge jimboni Sud-Ubangi kaskazini magharibi mwa Kongo. Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema wakimbizi 5,200 waliokuwa wakiishi Kongo walirejeshwa nchini mwao tangu Januari mwaka 2019.

Kwenye taarifa yake Jumapili, tume ya kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati,MINUSCA ilisema kwamba makundi ya waasi ya Anti-balaka, MPC, UPC, na rais wa zamani Francois Bozize ndio wanaohusika na machafuko ya hivi sasa nchini humo na watabeba dhamana na madhara yote kwa raia.