1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi washambulia kambi ya jeshi la angani Syria

MjahidA2 Agosti 2012

Huku mapigano yakiendelea kupamba moto nchini Syria rais wa Marekani asemekana kutia saini hati ya siri inayoonesha uungaji mkono wa nchi hiyo kwa waasi wa Syria

https://p.dw.com/p/15iTH
Mmoja wa waasi nchini Syria
Mmoja wa waasi nchini SyriaPicha: AP

Kifaru kilichoshikiliwa na waasi siku chache zilizopita ndicho kilichotumika kuishambulia kambi ya kijeshi ya Menagh mjini Allepo. Mwandishi wa habari wa shirika la AFP aliyeshuhudia mashambuluizi hayo amesema waasi walimwambia wamefanya hivyo kwa kuwa mara kwa mara ndege za kivita huruka kutoka kambi hiyo kuwashambulia wakaazi wa mji wa Allepo.

Jana Umoja wa Mataifa umethibitisha waasi wanaopambana na jeshi la Bashar al Assad sasa wana silaha nzito na kwamba waangalizi wa kijeshi wameshuhudia jeshi la Syria likiwashambulia waasi mjini Allepo.

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Reuters

Kwengineko mashambulizi yaliyofanywa na wanajeshi watiifu kwa Assad karibu na mji mkuu Damascus yamesababisha watu 43 kuuwawa. Wengi wa waliouwawa waliteswa, hii ni kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu Syria. Wanajeshi hao waliingia kwenye wilaya ya Jdaidet Artuz na kuwatia nguvuni vijana 100 kabla ya kuwapeleka katika shule moja kisha kuwatesa na wengine kuwauwa. Hii leo miili hiyo 43 ilipatikana ikiwa na alama za mateso.

Mashambulizi ya leo yamejiri wakati Rais wa Marekani Barrack Obama akiripotiwa kutia saini hati siri inayounga mkono mapigano ya waasi nchini Syria. Kulingana na kituo cha televisheni cha CNN, hati hiyo inatoa fursa kwa mashirika ya kijasusi na mashirika mengine kuwapa msaada wa kisiri waasi hao. Hata hivyo msaada kamili utakaotolewa na Marekani kwa waasi hao bado haujafafanuliwa.

Mikutano ya kusuluhisha mgogoro wa Syria

Kwengineko mkuu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa, Herve Ladsous, anatarajiwa hii leo jioni kuliarifu Baraza la Usalama la umoja huo juu ya hali halisi ya mambo nchini Syria. Zaidi ya watu 20,000 wameuwawa nchini humo na wengine 200,000 wakiachwa bila makao tangu kuanza kwa ghasia na maandamano ya kumuondoa Rais Bashar Al Assad madarakani.

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Reuters

Leo pia Waziri Mkuu wa Uingereza Davi Cameron na Rais wa Urusi Vladimir Putin wanatarajiwa kuwa na mazungumzo juu ya mzozo wa Syria.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky, amesisitiza kuwa Mkuu wake Ban Ki Moon anataka kuwepo kwa shinikizo la kimataifa kwa pande zote mbili ili kukomesha mapigano Syria. Siku ya Ijumaa Baraza la Umoja wa Mataifa litalipigia kura azimio la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu linalomtaka Rais Assad aachie madaraka.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef