Waasi wajiunga upya Mali
17 Aprili 2013Kuwasili kwa Pierre Buyoya kunafanyika siku moja tu, baada ya Ufaransa kupata rasimu ya azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuwepo kwa waalinzi 11,000 madhubuti wa amani, kwa ajili ya kuchukua majukumu ya kijeshi katika taifa hilo la Afrika magharibi kuanzia Julai mosi.
Mkuu huyo wa AFISMA, jeshi la nchi za Afrika la askari 6,000 linaloongoza katika operesheni ya Mali, ambae pia ni rais wa zamani wa Burundi alisema wamewasili katika mji huo wa Kidal kw ziara ya kikazi. Miongoni mwa mengine watajadili hali ya usalama na hatima ya majeshi ya Afrika sambamba na yale ya Ufaransa yalio katika uwanja wa mapambano.
Hali bado tete katika mji wa Kidal
Kidal ni mji tata uliyopo katika jiji lililobeba jina hilo hilo la Kidal katika eneo la jangwa, ambalo pia una milima ambayo imekuwa maficho ya wanamgambo wa kiislamu na ambalo pia kwa wiki kadhaa majeshi ya Ufaransa na Chad yanakibiliana na wanamgambo hao katika vita vya jangwani.
Baada ya kuondoshwa kwa mtutu wa bunduki katika iliyokuwa himaya yao maeneo ya miji ya kaskazini likiwemo jiji la Kidal, mapema Januari, wanamgambo wa kiislamu walikimbilia katika eneo la mbali la milima na kuanzisha vita vya jangwani dhidi ya mahasimu wao.
Akishangiliwa na umati wa wanajeshi wa Chad, Buyoya alitoa ahadi ya AFISMA kuendelea kusaidia wanajeshi hao kifedha, ambao amewasifu kwa kufanya kazi nzuri. Lakini mwishoni mwa juma rais wa Chad Idris Deby alitangaza kuwa jeshi hilo lipo tayari kuondoka nchini Mali baada ya kumaliza jukumu lao.
Wakati huohuo duru za kijeshi zinaonesha kuwa wanamgmabo hao wa kiislamu walijificha katika maeneo ya milima wameanza kujiunga upya wakiwa ndani ya taifa hilo na kwengineko.
Baada ya mashambulio makali kutoka kwa Ufaransa na Majeshi ya Mali tangu kuanza operesheni yao ambapo inadaiwa takribani wanamgambo 400 kuuwawa na wengine kadhaa kukimbilia katika milima ya kaskazini wa Niger na Chad, wengine kuvuka kusini mwa Libya na magharibi mwa Sudan wameanza kujiunga tena.
Mpaka sasa jiji la Kidal limekumbwa na matukio mawili ya miripuko ya mabomu Februari 21 na 26. Aprili 12 mwaka huu wanajeshi wanne wa Chad waliuwawa katika bomu la kujitoa mhanga lililoripuliwa katika soko moja katikati ya Kidal katika eneo ambalo jeshi la Afrika lilisema litaanza kuondoa vikosi vyake katika muda uliyopangwa.
Mwandishi Sudi Mnette
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman