Huku hayo yakiarifiwa mawakala kutoka asasi za kiraia wamedai hakuna mafanikio yoyote wakati huu ambapo mamia ya wananchi bado waendelea kuuawa na wengine kadhaa kuvitoroka vijiji vyao katika mikoa ya Kivu kaskazini na Ituri.
Akiuhutubia mkutano wa wandishi habari mwishoni mwa juma lililopita katika mji huu wa Goma,msemaji wa jeshi hapa kivu ya kaskazini amesifu kwanza juhudi za jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika operesheni zinazo lenga kuyatokomeza makundi ya waasi yanayo endesha mauwaji dhidi ya raia.
Tangu kutangazwa mamlaka ya kijeshi terehe 6 mei imekadiriwa, zaidi ya silaha 400 pamoja na wapiganaji 700 walijisalimisha mbele ya jeshi la Congo na takriban aslimia 90 ya vijiji vilivyo kuwa awali chini ya uongozi wa wanamgambo vimedhibitiwa na jeshi tiifu kwa serikali.
Mbali na tangazo hilo la maafisa wa jeshi hapa kivu ya kaskazini, miungano ya kiraia pamoja na mawakala wanao tetea haki za binadamu wamekua wakivishutumu vyombo vya usalama kufuatia ongezeko la visa vya uhalifu vinavyofanywa na makundi ya waasi.
Hata hivyo kulingana na ripoti iliyo tolewa mapema mwanzoni mwa wiki iliopita na shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch imekadiria kuwa watu wasio pungua 672 waliuawa katika mashambulizi yaliyoendeshwa na makundi ya wanamgambo tangu kutangazwa kwa serikali yakijeshi hadi septemba 10 mwaka huu.
Hali hii imewatia sasa wasiwasi mkubwa wananchi ambao baadhi wamesema wamepoteza matumaini yao kwa juhudi za utafutaji wa amani katika wilaya ya Beni na ndani ya maeneo kadhaa yanayo gubikwa na vurugu za vita.
Tangu kuwekwa kwa mamlaka yakijeshi katika mikoa ya kivu kaskazini na Ituri usalama wa wananchi bado unasalia kuwa tete nakuwafanya maelfu kutoroka miji na vijiji vyao ili kupata hifadhi ndani ya maeneo yanayo dhaniwa kuwa ni tulivu lakini bila msaada wa vyakula na maji safi.
Mhariri: Yusuf Saumu