Waasi wa Syria walitumia silaha za gesi ya Sarin yasema Urusi
10 Julai 2013Kwa mujibu wa Balozi Churkin, mashambulizi hayo yalifanywa tarehe 19 mwezi Machi kwenye eneo la Khan al-Assal nje kidogo ya mji wa Allepo unaodhibitiwa na serikali. Balozi huyo ameelekeza kidole cha lawama kwa wapiganaji wa upinzani kwa mashambulizi hayo yaliyowauwa watu 26 wakiwemo maafisa 16 wa usalama huku wengine 88 wakiwa wamejeruhiwa.
Lakini huku hayo yakiarifiwa waasi nao au wapiganaji wa upinzani wanailamu serikali kwa mashambulizi hayo.
Akizungumza na waandishi habari wakati alipokuwa akimkabidhi Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ripoti ya uchunguzi huo, Churkin amesema utawala wa Assad uliiomba Urusi ambaye ni mshirika wake wa karibu kufanya uchunguzi juu ya mashambulizi hayo baada ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kushindwa kuingia nchini humo kufuatia kutoelewana na Syria.
Balozi Churkin amesema kwa sasa majibu ya uchunguzi huo yanaonesha kuwa silaha zilizotumika hazikutengenezwa kiwandani na zilikuwa zimejaa gesi ya Sarin. Kukosekana kwa udhibiti wa kemikali inayohitajika katika kuiweka kwa muda mrefu inaonesha kwamba imetengenezwa katika siku za hivi maajuzi kwa hivyo kulingana na Churkin hii moja kwa moja inaonesha waasi ndio waliotumia silaha hizo za kemikali katika mashambulizi ya Khan al-Assal
Ban Ki Moon ataka ushahidi zaidi
Hata hivyo Uingereza, Ufaransa na Marekani sasa zimewasilisha ripoti tofauti kwa Umoja wa Mataifa inayozungumzia mashambulizi ya silaha za kemikali nchini Syria.
Marekani inasema inaamini kwamba vikosi vya serikali ya Bashar Al Assad vimewauwa zaidi ya watu 150 kwa kutumia gesi ya Sarin. Kwa upande wake Ban Ki Moon amesema anataka ushahidi zaidi juu ya hilo na sio tu katika eneo moja la Khan al-Assal.
Matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria imevuka mpaka aliouweka Rais wa Marekani Barrack Obama wa kutojiingiza moja kwa moja katika mgogoro wa Syria unaoendelea kwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Kando na kutuma misaada ya kibinaadamu Marekani imekuwa na wazo la kutuma silaha kwa waasi wa Syria. Tangu kuanza kwa ghasia hizo takribani watu 93,000 wameshauwawa, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef