Waasi wa M23 warejea Congo
16 Januari 2017Karibu wapiganaji 200 wa kundi la M23 , kundi la Watutsi walio jamii ya wachache lililoshindwa na jeshi la Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo miaka mitatu iliyopita , wamewasili kutoka Uganda na kukamata kijiji kimoja kaskazini mwa jimbo la Kivu ya kaskazini, msemaji wa serikali ya Congo Lambert Mende ameliambia shirika la habari la Ufaransa afp.
Mende amesema jeshi la Congo linapambana na vikosi viwili vilivyopelekwa katika kijiji cha Ishasha ambavyo vilitarajiwa kuwa nchini Uganda chini ya uangalizi wa maafisa wa nchi hiyo.
"Ni vipi majirani zetu wa Uganda , ambao tuna mipaka nao wakiwajibika kabisa, wameweza kuruhusu watu ambao walikuwa wanaishi katika makambi ya wakimbizi kuvuka mpaka na silaha , hadi katika ardhi yetu?" ameongeza.
Serikali ya Congo imesema jenerali wa zamani wa jeshi, Sultani Makenga , anaongoza moja kati ya batalioni. Hakuna msemaji wa jeshi alipatikana kuthibitisha mapigano hayo na kundi la M23. Omar Kavota, mkurugenzi wa kituo cha kuhimiza amani , demokrasia na haki za binadamu amesema Jumapili kwamba vyanzo katika kijiji cha Ishasha vimethibitisha kuwapo kwa wapiganaji wa kundi la M23 lakini amesema "hakukuwa na mapigano ama mapambano bado".
Hatari ya mapigano
Majimbo yenye utajiri mkubwa wa madini nchini Congo yameathirika na miaka kadhaa ya mzozo mbaya kabisa, wakati mataifa jirani yakiunga mkono makundi ya waasi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya mamlaka ya mjini Kinshasa, na sasa wanamgambo wanaotembea hovyo katika eneo hilo wanazusha mapigano makubwa na kuwatisha raia.
Baada ya kushindwa katika mapigano ya mwaka 2013 na jeshi la Congo na majeshi ya Umoja wa mataifa , kundi la M23 lilikubali mpango wa kuweka silaha chini na kunyang'anywa silaha, kuvunja vikosi vyao na kujumuishwa katika jamii ya watu wa Congo.
Lakini kurejea kwa waasi hao wa zamani kulikwama , ambapo chini ya wapiganaji 200 kati ya wapiganaji karibu 1,900 waliokuwa wakihifadhiwa nchini Uganda na 13 kati ya mamia waliondoka nchini Rwanda na kurejea Congo.
Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Congo maafisa waliishutumu Rwanda na Uganda kwa kuruhusu waasi kutumia ardhi zao kama sehemu ya kuanzisha mashambulizi yao. Hivi karibuni kabisa, wameyalaumu mataifa hayo kwa kuwa na nia mbaya ya kuwaruhusu wahalifu kutembea huru kabisa , badala ya kuwarejesha ili kufikishwa mahakamani nchini Congo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uganda Henry Okello Oryem , akizungumza na shirika la habari la afp mjini Kampala , alikana vikali kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao wamevuka mpaka.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afp
Mhariri: Idd Ssessanga