Waasi wa M23 wakutana na Kabila
25 Novemba 2012Wakipata ushindi mdogo kwa viongozi hao wa kimkoa, kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo la waasi wa mashariki ya jamhuri ya Congo Jean -Marie Runiga Lugerero , amesema kuwa alikuwa na mazungumzo ya awali na Kabila baada ya mkutano huo uliofanyika mjini Kampala kumalizika.
Wakati hakualikwa binafsi katika mkutano huo , Runiga Lugerero aliliambia shirika la habari la AFP kuwa alifanikiwa kukutana na Kabila kwa kupitia upatanishi wa rais wa Uganda Yoweri Museveni, ambae alitarajiwa kufanya nae mazungumzo hii leo Jumapili(25.11.2012).
"Hali ilikuwa tete lakini baadaye , kila upande ulipunguza jazba katika majadiliano kwasababu haya si matatizo ya kibinafsi , lakini ni matatizo ya nchi" ambayo inapaswa kupatiwa ufumbuzi, ameliambia shirika la habari la AFP kwa simu.
"Nafikiri mkutano huo ulikwenda vizuri sana".
Runiga Lugerero na Kabila watakutana tena leo Jumapili(25.11.2012) kujadiliana juu ya vipi mazungumzo yao yatakavyoendelea, ameongeza.
"Ndio walikutana," Waziri wa mambo ya kigeni wa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo Raymond Tshibanda ameliambia shirika hilo la habari. Lakini amekanusha kuwa mazungumzo zaidi ya ana kwa ana kati ya Kabila na kundi la M23 yanatarajiwa.
Tangazo la Runiga Lugerero limekuja siku chache baada ya Kabila kuonekana kuondoa uwezekano wa mazungumzo na majeshi hayo ya waasi.
Na saa chache hapo kabla , katika tamko lao la kufunga kikao , viongozi wa kimkoa wametoa wito kwa wapiganaji wa kundi la M23 kusitisha mapigano na kuondoa majeshi yao katika mji muhimu wa mashariki wa Goma katika muda wa saa 48.
Runiga Lugerero , hata hivyo , ameweka wazi kuwa hatua yoyote ya kuondoa majeshi itakuja pale tu baada ya mazungumzo kati ya kundi hilo la waasi na Kabila. Wapiganaji wa M23 watalinda maeneo yao iwapo majeshi ya Congo yatashambulia, ameonya.
Kagame hakuhudhuria
Mkutano huo hata hivyo haukuhudhuriwa na rais wa Rwanda Paul Kagame. Maafisa wa Uganda wametangaza hapo mapema Jumamosi kuwa Rwanda badala yake itawakilishwa na waziri wa mambo ya kigeni Louise Mushikwabo.
Kagame amekuwa akikana shutuma , sio tu kutoka jamhuri ya kidemokrasi ya Congo lakini pia kutoka kwa wachunguzi wa umoja wa mataifa , kuwa Rwanda inawaunga mkono , na kuliendesha jeshi la waasi la M23 ambalo wengi wao ni kutoka kabila la Watutsi.
Waasi watakiwa kusitisha mapigano
Katika taarifa yao ya pamoja mwishoni mwa kikao chao , viongozi wa kimkoa wamelitaka kundi la waasi la M23 , "kusitisha shughuli zote za kivita", na "kuacha kusema kuwa wanataka kuiangusha serikali iliyochaguliwa ya Congo." Siku ya Jumatano, (21.11.2012), Vianney Kazarama, mmoja kati ya viongozi wa waasi, amesema kuwa Kabila ni lazima aondoke madarakani.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uganda Sam Kutesa amesema kuwa mkutano huo umetoa wito kwa waasi kuondoka kutoka mjini Goma na kurejea katika eneo karibu kilometa 20 kaskazini mwa mji huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Bruce Amani