1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa LRA wasaini mkataba na serikali ya Uganda

Josephat Charo24 Februari 2008

Mkataba wa mwisho kusainiwa katika siku chache zijazo

https://p.dw.com/p/DCPv
Mwanajeshi kijana wa kundi la LRA Samuel Okumu akiwa na bunduki lake katika mpaka wa Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: AP

Kundi la waasi wa Lord´s Resistance Army, LRA, limesaini mkataba wa kudumu na serikali ya Uganda wa kusitisha mapigano, katika hatua nyengine muhimu kuelekea kufikiwa kwa mkataba wa mwisho wa amani.

Pande hizo mbili zilisaini mkataba huo wakati wa mazungumzo ya amani katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Msemaji wa ujumbe wa serikali ya Uganda katika mazungumzo hayo, Chris Magezi, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuumaliza mzozo wa kaskazini mwa Uganda.

Mkataba huo utaanza kutekelezwa siku moja baada ya mkataba wa mwisho kusainiwa kati ya waasi wa LRA na serikali ya Uganda. Wapatinishi katika mazungumzo ya amani ya mjini Juba wanasema wana matumaini mkataba wa mwisho utasainiwa katika siku chache zijazo.

Joseph Ochieno wa chama cha Uganda People´s Party amesema hii ni siku nzuri kwa Uganda na kwa watu wote wanaopigania amani badala ya vita.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo ya mjini Juba, rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano, amethibitisha kwamba mkataba huo una maana kwamba vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Uganda vilivyodumu miongo miliwi vimefika mwisho.