Waasi wa kundi la SLA wasema hawatahudhuria mkutano wa Arusha
2 Agosti 2007Makamanda wa kundi kubwa la waasi la Sudanese Liberation Army, SLA, wamesema hawatahudhuria mkutano wa mjini Arusha nchini Tanzania utakaojadili mchakato wa kutafuta amani baina ya serikali ya Sudan na waasi wakitaka kiongozi wao wa ngazi ya juu, Suleiman Jamous, aruhusiwe kuhudhuria mkutano huo.
Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika ziliyaalika makundi ya waasi katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan ambayo hayakusaini mkataba wa amani na serikali ya Sudan yahudhurie mazungumzo ya kutafuta amani Jumapili ijayo mjini Arusha. Lengo la mkutano huo ni kuhakikisha pande zote husika zinajumulishwa kwenye mashauriano na mipango ya mazungumzo ya kutafuta amani kati ya waasi na serikali ya mjini Khartoum na kuzuia diplomasia ya kuwekeana muda.
Suleiman Jamous, mratibu wa maswala ya kibinadamu wa kundi la Sudanese Liberation Army, amekuwa kama mtu aliye kifungoni katika mji wa Kordofan karibu na Darfur, kwa kipindi cha miezi 13 baada ya kulazwa katika hospitali ya Umoja wa Mataifa iliyo mjini humo ili atibiwe. Serikali ya Sudan imesema itamtia mbaroni kiongozi huyo mara tu atakapoondoka kwenye hospitali hiyo.
Wiki hii watetezi 11 mashuhuri wakiwemo askofu mkuu wa Afrika Kusini, Desmond Tutu, balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Richard Holbrooke, rais wa zamani wa jamhuri ya Ucheki, Vaclav Havel, na mshindi wa tuzo ya Nobel, Jody Williams, walimuandikia barua rais wa Sudan, Omar Hassan el Bashir wakimuomba amuachilie huru Suleiman Jamous.
Wadadisi wa maswala ya kisiasa wanasema Suleiman Jamous ni kiungo muhimu kati ya waasi na operesheni kubwa ya utoaji misaada ya kibinadamu katika jimbo la Darfur, ambayo imelazimika kupungua kutokana na mashambulio ya waasi dhidi ya misafara ya magari inayopeleka misaada kwa wakaazi wa jimbo hilo. Inakadiriwa watu takriban nusu milioni hawawezi kufikishiwa misaada kwa sababu ya hali mbaya ya usalama.
Wachambuzi pia wanasema Suleiman Jamous ana ushawishi mkubwa wa kuweza kuyaunganisha makundi mbalimbali ya waasi na makanda wa jeshi katika jimbo la Darfur na utawala wa kisiasa nje ya jimbo hilo, jambo ambalo ni kikwazo kikubwa katika kuutanzua mzozo wa Darfur kwa njia ya amani.
Kiongozi wa kitengo cha kundi la Sudanese Liberation Army, Abdallah Yehia, amesema na hapa namnukuu, ´Makanda wetu wanasema hatutakwenda Arusha ikiwa Jamous hatakwenda´, Kiongozi huyo amesisitiza umuhimu wa Suleiman Jamous kuhudhuria mkutano wa mjini Arusha. Abdalla Yehia anasema ameuambia Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuhusu swala hilo lakini viongozi wa jumuiya hizo wanasema ni vigumu.
Abdalla Yehia anauliza, haiwezekani vipi kumruhusu Jamous kwenda Arusha ilhali yuko katika hospitali ya Umoja wa Mataifa huko Kordofan? Hata hivyo amethibitisha atahudhuria mkutano wa mjini Arusha, ingawa makamanda wa kundi la SLA hawatakwenda.
Julie Flint, mwandishi aliyechangia katika kuandika kitabu kuhusu Darfur anasema kundi la SLA ni muhimu katika mazungumzo ya kutafuta amani kwani linadhibiti eneo kubwa la kaskazini mwa jimbo la Darfur pamoja na sehemu kadhaa za mashariki na kusini mashariki mwa jimbo hilo.
Umoja wa Mataifa haujasema lolote kuhusu uamuzi wa kundi la SLA kutohudhuria mkutano wa mjini Arusha.
Juzi Jumatano serikali ya Sudan ilisema iko tayari kumuachia Jamous lakini ikasema mjumbe maalumu wa Umoja wa mataifa katika jimbo la Darfur, Jan Eliasson na mwenzake wa Umoja wa Afrika, Dr Salim Ahmed Salim, hawajaliwasilisha swala hilo kwenye mazungumzo.
Jan Eliasson na Dr Salim Ahmed Salim wanajukumu la kusimamia mchakato mzima wa amani katika jimbo la Darfur na wataongoza mkutano unaoanza leo mjini Arusha Tanzania.