1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Kihouthi waenda Sweden kwa mazungumzo ya amani

Sekione Kitojo
4 Desemba 2018

Ujumbe wa waasi umeondoka katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa ukielekea katika mazungumzo muhimu nchini Sweden pamoja  na  wawakilishi wa serikali mazungumzo yenye lengo la kumaliza vita vilivyoiharibu nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/39Rsb
Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Picha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Safari  ya  wapiganaji  hao wa  Kihuthi  inafuatia  makubaliano  ya  kubadilishana  wafungwa pamoja  na  kuondolewa kwa  waasi  50  waliojeruhiwa kwenda kupata  matibabu  nchini  Oman  katika  hatua  muhimu  ya kuimarisha  juhudi  hizo  za  amani.

Ujumbe huo  umeongozana  na  mjumbe  maalum  wa  Umoja  wa Mataifa  Martin Griffiths , kimesema  chanzo  katika  uwanja  wa ndege. Msemaji  wa  waasi  Mohammed Abdelsalam  amethibitisha kuondoka  kwao  katika  maelezo  aliyoyatoa  katika  ukurasa  wa Twitter, akisema  Wahuthi  hao  "hawataacha  juhudi  za  kuyafanya mazungumzo  hayo  ya  mafanikio  ili  kurejesha  amani  na  kumaliza matumizi  ya  nguvu  na  uchokozi".

Wakati  huo  huo  aliwataka  wapiganaji  wa  waasi  kuendelea kubakia  waangalifu  dhidi  ya  juhudi  zozote zitakazo  chochea hatua  za  kijeshi".

Licha  ya  kwamba  hakuna  tarehe  kamili  iliyotangazwa  kwa  ajili ya  kuanza  mazungumzo  hayo, duru  za  serikali  ya  Yemen zinasema  mazungumzo  hayo  yanaweza  kuanza  siku  ya  Alhamis.

Jemen Militär starte Offensive gegen Houthi-Rebellen ARCHIV
Wapiganaji wa Kihouthi nchini YemenPicha: picture alliance/dpa/Str

Waziri  wa habari  na  msemaji wa  Wahothi  mjini  Sanaa  Daifallah Al-Shami  hapo  kabla  alisema kwamba  pamoja  na  kuelekea  huko nchini  Sweden  lakini  hawajapata  mualiko  rasmi.

"Hadi  sasa  hatujapata  mwaliko  wowote  moja  kwa  moja kutoka  Umoja  wa  mataifa  kwa  ajili  ya  mazungumzo  hayo nchini  Sweden. Kutokana  na  juhudi za  Umoja  wa  mataifa  na mjumbe  wake  maalum ,  hatuwezi  kuona  mwelekeo  wa  wazi kwa  ajili  ya  mazungumzo  hayo."

Makubaliano  ya  kubadilishana  mamia  ya  wafungwa yalikaribishwa na  kamati  ya  kimataifa  ya   shirika  la  msalaba  mwekundu, shirika ambalo  litaangalia  mabadilishano  hayo  baada  ya  duru  ya kwanza  ya  mazungumzo  yaliyopangwa  ya  amani  nchini  Sweden. 

Makubaliano  hayo  yalifikiwa  kwa  upatanishi  wa  Griffiths, ambaye alikuwa  katika  mji  mkuu  unaoshikiliwa  na  waasi  wa  Sanaa  kwa ajili  ya  mikutano   ambayo  tayari  ilikwisha  tiwa  shime  na kuondolewa  kwa  wapiganaji  ambao  walikuwa  wamejeruhiwa, sharti  moja  muhimu  la  waasi  kwa  ajili  ya  mazungumzo  hayo.

Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika Yemen Martin GriffithsPicha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Juhudi  za  awali  za  Umoja  wa  mataifa  kufanya  upatanishi  na kuwaleta  pamoja  Wahuthi  na  serikali  inayoungwa  mkono  na Saudi  Arabia  katika  meza  ya  majadiliano  zilivunjika  nchini  Uswisi mwezi  Septemba.
 

Umoja  wa  Falme  za  Kiarabu , nchi  nyingine  muhimu  inayounga mkono  serikali  ya  nchi hiyo, imesema  mazungumzo  hayo yaliyopangwa  yanatoa  fursa  muhimu , ya  kumaliza  karibu  miaka minne  ya  vita.

Mwandishi: Sekione  Kitojo  / afpe

Mhariri: Mohammed Khelef