Waasi wa Houthi kusitisha mapigano Yemen
19 Novemba 2018Taarifa iliyosainiwa na kiongozi wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Houthi, Mohammed Ali al-Houthi na kuchapishwa mapema leo katika ukurasa wa Twitter wa kundi hilo, imeeleza kuwa waasi hao wako tayari kusitisha mapigano kama majeshi ya Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na washirika wake yanataka amani.
Hatua hiyo imetangazwa, wakati ambapo jumuia ya kimataifa inaongeza shinikizo la kuzitaka pande zinazohasimiana kusitisha vita vya Yemen ambavyo vimedumu kwa karibu miaka minne, huku mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Martin Griffiths akijaribu kuitisha awamu mpya ya mazungumzo ya amani yatakayofanyika nchini Sweden.
Tarehe rasmi ya mazungumzo hayo bado haijatangazwa, ingawa Griffiths amesema itakuwa hivi karibuni. Mazungumzo mengine ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa kati ya serikali ya Yemen na waasi wa Houthi yalivunjika mwezi Septemba.
Al-Houthi pia ameyatolea wito makundi mengine ya waasi kusitisha mashambulizi dhidi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia, ili kuonesha ushirikiano na kuupokonya muungano huo haki ya kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya vikosi vya Houthi.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Yemen, Mohamed Shamsan anasema wito wa kuanzisha mazungumzo ya amani umekuwa ukitolewa, ingawa operesheni za kijeshi zinaendelea.
''Pande zote zinazohasimiana zimetoa wito wa kuanzisha haraka iwezekanavyo mazungumzo ya amani, lakini shughuli za kijeshi zimeendelea kuongezeka na kuwa mbaya zaidi. Hii ni kwa sababu pande zinazohasimiana zinataka kuwa na mamlaka zaidi katika mazungumzo yajayo ya amani kupitia operesheni za kijeshi,'' alisema Shamsan.
Muungano huo wa kijeshi uliongeza mashambulizi katika mji muhimu wa Hodeida, licha ya kuwepo jaribio la hivi karibuni la kusitisha mapigano. Hata hivyo, mbali na kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, Ijumaa iliyopita waasi walisema kuwa kiasi ya raia 10 waliuawa na mashambulizi yaliyofanywa na majeshi ya muungano yanayoongozwa na Saudi Arabia mjini Hodeida.
Vita vya Yemen vimewaua zaidi ya watu 10,000, ingawa wanaharakati wanaamini kwamba idadi ya watu waliouawa inaweza kuwa ya juu zaidi. Aidha, kufungwa kwa bandari muhimu ya Hodeida kunaweza kusababisha baa la njaa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga