1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa FARC kusaini makubaliano ya amani

26 Septemba 2016

Colombia itapiga hatua kubwa kuelekea kuliepuka jinamizi la muda mrefu la machafuko wakati serikali na kundi la waasi nchini humo watakaposaini mkataba wa amani uliopatikana baada ya miaka minne migumu ya mazungumzo 

https://p.dw.com/p/2QaCj
Kolumbien FARC Friedensvertrag
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Mazalan

Umuhimu wa muafaka huo ni mkubwa mno: mgogoro wa Colombia uliodumu kwa zaidi ya miongo mitano, kwa sehemu ukichochewa na biashara ya dawa za kulevya aina ya cocaine, umeua zaidi ya watu 220,000 na kuwaacha wengine milioni 8 bila makaazi. Ili kuonyesha umuhimu wa siku hii, mkataba huo utasainiwa na Rais wa Colombia Juan Manuel Santos na kamanda mkuu wa Revolutionary Armed Forces of Colombia – FARC, mpiganaji muasi anayefahamika kwa jina la utani la Timochenko. Akizungumza katika mkesha wa siku hii, Rais Santos amesema "Nadhani juhudi zote zilikuwa muhimu na sasa tunastahili kufanya juhudi kubwa zaidi ili kuufanikisha mkataba huu kwa sababu hatuna kikwazo mbele yetu. Natumai kwa pamoja, sote, yani wale wanaounga mkono kura ya "Ndiyo" na wale wenye wasiwasi..kuwa tunaweza kuungana baada ya kura ya maoni kupita na tunaweza kuitengeneza nchi mpya pamoja".

Marais 15 wa Amerika Kusini, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry wanatarajiwa kushuhudia tukio hilo la kihistoria katika mji wa kikoloni wa Cartagena.

Kolumbien Präsident Juan Manuel Santos
Rais wa Colombia Juan Manuel Santos akiidhinisha makubaliano ya amani na FARC mnamo 30.08.2016Picha: picture-alliance/dpa/L. Munoz

Zaidi ya wageni 2,500 walioalikwa kwenye sherehe hiyo wametakiwa kuvalia nguo nyeupe kama ishara ya amani, na Santos atautia saini mkataba huo wa kurasa 297 kwa kutumia kalamu iliyotengenezwa na ganda lililotumika vitani.

Kutiwa saini mkataba huo hakutakuwa mwisho wa mambo hata hivyo. Wacolombia wanapewa fursa ya kuwa na usemi wa mwisho wa kuidhinisha au kupinga mkataba huo katika kura ya maoni ya Oktoba 2. Uchunguzi wa maoni unaonyesha ushindi wa kura ya "ndiyo”, lakini baadhi ya wachambuzi wanaonya kuwa idadi ndogo ya wapiga kura huenda ukawa habari mbaya kwa changamoto nyingi zinazoikabili nchi hiyo katika utekelezaji wa muafaka huo muhimu.

Miongoni mwa hatua kubwa na zenye utata zaidi itakuwa ni kuzifungua kesi za uhalifu wa kivita dhidi ya waasi na wahusika wa serikali. Chini ya kanuni za mkataba huo, waasi watakaoweka chini silaha zao na kukiri makosa yao watasamehewa kifungo cha jela na kutakiwa kuwafidia waathiriwa kwa kufanya kazi ya maendeleo katika maeneo yaliyoathirika pakubwa na mgogoro huo.

Serikali pia imeahidi kushughulikia suala la ugawaji usiokuwa wa usawa wa mashamba, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likizungumziwa na FARC tangu kundi hilo lilipoanzishwa kama jeshi la wakulima wadogowadogo mwaka wa 1964, na serikali ilikubali kushirikiana na waasi ili kuwapa maendeleo mbadala maelfu ya familia zinazotegemea biashara ya cocaine. Kama mkataba huo utaidhinishwa na kura ya maoni, basi wapiganaji karibu 7,000 wa FARC wataanza kuhamishwa hadi maeneo 28 katika kipindi cha miezi sita ijayo ambapo watasalimisha silaha zao kwa waangalizi watakaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga