1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa CODECO waua zaidi ya watu 20 nchini Kongo

Sylvia Mwehozi
22 Juni 2024

Zaidi ya raia 20 wameuawa na waasi wa kundi la Codeco katika kijiji kimoja kwenye mkoa wenye utajiri mkubwa wa dhahabu wa Ituri huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4hNt4
Majeneza kwenye moja ya mashambulizi ya waasi Kongo
Makundi ya waasi yanayoendesha mashambulizi yake mashariki mwa Kongo yamekuwa yakisababisha vifo vya raia wasio na hatia kila uchao.Picha: Jorkim Jotham Pituwa/AFP via Getty Images

Afisa tawala katika eneo la Banyali Kilo, Innocent Matukadala amelieleza shirika la habari la AFP kwamba wanamgambo wa Codeco, walivamia kijiji cha Lodjo siku ya Alhamisi na kuwaua watu wanane na kisha kurejea siku ya Ijumaa na idadi ya vifo ni 36.

Afisa huyo aliongeza kuwa jeshi la Kongo lilifika kwa kuchelewa kuzuia mauaji na kwamba wakaazi wamefikwa na taharuki.

Kiongozi mwingine wa asasi ya kiraia aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa majina alisema watu waliouawa ni 28 na wengi wameyakimbia makazi yao. Vyanzo vingine vimeitaja idadi ya watu waliouawa kuwa ni 23.