1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Chad wasema wako tayari kusitisha mapigano

Zainab Aziz Mhariri: Saumu Njama
25 Aprili 2021

Waasi waliofanya mashambulizi mkubwa kaskazini mwa Chad wiki mbili zilizopita na ambao wamelaumiwa na jeshi kwa kumuua mtawala mkongwe wa nchi hiyo Idriss Deby Itno, wamesema sasa wako tayari kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/3sXMA
Rebellen in tschadische Hauptstadt N'Djamena eingerückt
Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, kiongozi wa kundi la waasi la Front for Change and Concord in Chad (FACT) Mahamat Mahadi Ali alitoa kauli hayo siku ya Jumamosi. Alipozungumza na waadhishi wa habari wa shirka la AFP akiwa mjini Libraville, Gabon, kiongozi huyo wa waasi alisema licha ya wao kuthibitisha kwamba wako tayari kufanikisha upatikanaji amani, kwa kusitisha mapigano, wameshambuliwa na vikosi vya serikali ya Chad.

Kiongozi huyo wa kundi la waasi wa FACT Mahadi Ali amesisitiza kuwa hatua za kusitisha mapigano zinapaswa kuzingatiwa na pande zote mbili. Amesema hawatoweza kukunja mikono yao na kuruhusu wauawe.

Rais wa Chad aliyeuawa Idriss Deby
Rais wa Chad aliyeuawa Idriss DebyPicha: Lemouton Stephane/ABACA/picture alliance

Kundi hilo la waasi ambalo lilianzisha mashambulizi dhidi ya utawala wa nchini Chad kutokea nchi jirani ya Libya wiki iliyopita lilitoa vitisho mnamo siku ya Jumanne kwamba lingeelekea katika mji mkuu N'Djamena baada ya kifo cha rais Idriss Deby Itno, sababu ikiwa ni kupinga kuongozwa na mmoja wa watoto wa Deby. Kauli hiyo ilitolewa na msemaji wa kundi hilo la waasi la Front for Change and Concord in Chad (FACT), Kingabe Ogouzeimi de Tapol.

Kwa upande wa serikali ya Chad, msemaji wa baraza la kijeshi linaloongozwa na mwanawe marehemu aliyekuwa rais wa Chad Idriss Deby ambaye ndiye mrithi wake, Mahamat Idriss Deby, amesema, kwa kuwa kundi la FACT ni la waasi, ndiyo sababu wanawashambulia kwa mabomu. Kwa ufupi wamo katika vita na kundi hilo la waasi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Christophe P. Tesson/Epa/AP/picture alliance

Ufaransa na washirika wake wa kikanda wameonyesha kumuunga mkono Mahamat Idriss Deby. Siku ya Ijumaa, Chad ilifanya mazishi ya kiserikali ya kiongozi wake aliyeuawa Idriss Deby Itno, aliyeongoza mapambano dhidi ya makundi ya waasi katika eneo la Sahel. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, katika hotuba yake kuhusu rais wa Chad aliyeuawa, alimtaja kiongozi huyo kama shujaa na alisema: "Uliishi kama askari, umekufa kama askari, silaha mikononi mwako".

Macron ameahidi kusimama na Chad na amesema Ufaransa kamwe haitamruhusu mtu yeyote, kuvuruga utulivu na uadilifu wa Chad na ameutaka utawala wa kijeshi ulioteuliwa hivi karibuni kuendeleza amani na utulivu, kuchagua njia ya kuwajumuisha wadau mablimbali, kufanya mazungumzo na kuzingatia hatua zote za kidemokrasia katika kipindi cha mpito.

Chanzo. AFP