1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa ADF wauwa tena mashariki mwa DRC

2 Septemba 2021

Siku chache baada ya hali ya dharura kuongezewa muda kwa mara ya saba mfululizo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, waasi wa ADF wameshambulia tena na kuuwa watu wanne na kuchoma moto magari 16 mkoani Ituri.

https://p.dw.com/p/3zoIG
Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Waasi wa ADF wanaoaminika kuwa wanatoka Uganda walishambulia msafara wa mamia ya magari uliokuwa unalindwa na jeshi la Umoja wa Mataifa pamoja na jeshi la Kongo katika kijiji cha Ofaya mkoani Ituri siku ya Jumatano (Septemba 1).

Kwenye mashambulizi hayo, watu wanne waliuawa, zaidi ya 90 kutekwa nyara na magari 16 kuchomwa moto.

Mashambulizi hayo yamewakera wakaazi wa eneo hilo, ambao wameshapoteza imani ya kuona amani inarudi.

Mashambulizi hayo makubwa ya aina yake, yalitokea siku chache tu, baada ya utawala wa hali ya dharura kuongezewa muda zaidi katika mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri. 

Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Wanajeshi wa jeshi la taifa la Kongo wanaopambana na waasi wa ADF mashariki mwa nchi hiyo.Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Wasafiri walionusurika walisema kwamba ADF walifanikiwa kuvamia msafara wa magari zaidi ya 100 yaliyokuwa yanasindikizwa na majeshi ya ya Umoja wa Mataifa (MONUSCO) pamoja na jeshi la Kongo (FARDC) na kupora bidhaa kabla ya kuchoma moto magari hayo 16, mawili kati yao yakiwa malori ya mizigo.

Hata hivyo, jeshi la FARDC liliwaandama waasi hao walipokuwa wakielekea misituni na mateka wao na kufanikiwa kuwaokoa baadhi ya mateka, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Kongo katika mkoa wa Ituri, Luteni Jules Ngongo.

"Baada ya adui kuchoma magari, majeshi yaliingilia kati kupambana na adui na kipaumbele kwetu ilikuwa ni kuwaokoa mateka na wakati huu jeshi limefanikiwa kuwaokowa mateka zaidi ya sitini," aliongeza Luteni Ngongo.

"Uzembe" wa utawala wa dharura, wadai wananchi

Symbolbild | DR Kongo | Anschlag der Alliierte Demokratische Kräfte Kongo
Wanajeshi wa jeshi la taifa la Kongo wanaopambana na waasi wa ADF mashariki mwa nchi hiyo.Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mashambulizi haya yametokea wakati kuna vuta ni kuvute baina ya viogozi wa serikali kuu mjini Kinshasa na wakaazi wa maeneo yaliyo chini ya utawala wa dharura, kuhusu kile wanachosema wakaazi hao kuwa ni "uzembe katika utendaji kazi wa viongozi" wa maeneo hayo.

Mashirika ya kutetea haki za binaadamu pia yamelaani vikali vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na waasi wa ADF.

Hata hivyo, mwanasheria Omar Kavota, ambaye ni naibu mwenyekiti wa shirika la CEPADHO, aliwaomba wakaazi waliokata tamaa kuendelea kuwa na matumaini huku akiiomba serikali kufanya juu chini kuwatokomeza waasi wa ADF.

Lakini wakati zaidi ya watu 20 wakipoteza maisha kwenye mashambulizi mbalimbali ya ADF ndani ya kipindi cha wiki moja, imani ya kuwaona waasi hao wanatokomezwa inaonekana kutoweka. 

Imeandikwa na John Kanyunyu/DW Beni