Waasi Libya wanaendelea kumsaka Gaddafi
9 Septemba 2011Waasi hao wameweka vituo hivyo vya wapiganaji kunasa mawasiliano ya simu ya kiongozi huyo wa zamani, kujaribu kumtafuta alikojificha.
Wakati huo huo baraza la kitaifa la waasi nchini humo, limeonya kuwa vita vya kuikomboa Libya bado havijamalizika.
Kituo cha televisheni cha Al Arabiya kimemnukuu msemaji wa baraza la jeshi mjini Tripoli, Anis Sharif akisema kuwa waasi nchini humo wana kikosi maalumu cha wanajeshi 200 kinachoongoza msako huo dhidi ya kiongozi wa zamani, Muammar Gaddafi.
Sharif amesema waasi wametambua sehemu aliko Gaddafi lakini hakusema ni wapi. Ameongeza kuwa kukamatwa kwake ni suala la muda tu.
Kiongozi huyo wa zamani wa Libya anaaminika kujificha katika mojawapo ya maeneo matatu ambayo bado wafuasi wake wanayadhibiti, mji alikozaliwa Sirte, Mji wa Bani Walid kusini mashariki mwa mji mkuu Tripoli, au mji wa Sabha, katika jangwa la kusini.
Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Al jazeera, hii leo waasi walisogea karibu na mji wa Sirte na Bani Walid saa kadhaa kabla ya kumalizika muda wa mwisho uliotolewa kwa wafuasi wa Gaddafi kujisalimisha au wakabiliwe na mashambulio ya kuwamaliza.
Kiasi ya waasi 12 waliuawa katika mapigano na vikosi vinavyomuunga mkono Gaddafi nje ya mji wa al Wadi al Ahmar kiasi ya kilomita 60 mashariki mwa mji ulioko pwani, Sirte.
Hapakuwa na ripoti za watu waliojeruhiwa miongoni mwa vikosi vya Gaddafi.
Wakati huo huo baraza la kitaifa la waasi nchini Libya limewatuma wanajeshi zaidi katika mji uliozungukwa wa Bani walid, wakati majadiliano na viongozi wa makabila yakiwa bado hayajafaulu. Katika hotuba yake ya kwanza mjini Tripoli, kiongozi wa sasa wa Libya, Mahmud Jibril ameonya kwamba mapigano makali yanatarajiwa wakati wapiganaji watiifu kwa watawala wapya wakiukaribia mji wa Sirte.
Hapo jana jioni, Jibril alisema kuwa vita vya kujikomboa bado havijakamilika, na kuongeza kuwa vitakamilika pale Gaddafi atakapokamatwa.
Katika jitihada za kuzifunga njia za Gaddafi kutoweka, baraza hilo la waasi limesema limetuma kikosi katika mji mkuu wa Niger, Niamey na Marekani imesema wasaidizi wa Gaddafi waliokimbilia Niger wanazuiliwa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Victoria Nuland, ameeleza kuwa wale wote walioingia Niger mapema wiki hii hawamo katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa.
Marekani pia imewasiliana na Mali na Mauritania, Chad na Burkina Faso kusisitiza umuhimu wa kuheshimu maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa, na umuhimu wa kuimarisha usalama katika mipaka ya nchi hizo.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International, limesema nchi jirani na Libya lazima zimkamate Gaddafi, na wengine wanaosakwa na mahakama ya uhalifu wa kivita, ICC, iliyopo mjini The Hague Uholanzi, iwapo watavuka mipaka ya nchi hizo.
Mwandishi Maryam Abdalla/ Dpae/afpe
Mhariri:Josephat Charo