Waasi Libya wadai mtoto wa Gaddafi ameuawa
5 Agosti 2011Msemaji huyo wa waasi wa Libya Mohammed Zawawi,amesema kuwa Khamis Gaddafi ambaye alikuwa miongoni mwa watu 32 waliyouawa katika shambulizi hilo, alikuwa ni mmoja wapo wa makamanda wa juu wa jeshi la Gaddafi.
Hata hivyo maafisa wa NATO wamesema wamesikia juu ya taarifa hizo, lakini hawawezi kuthibitisha, kwani hawana mtu yoyote katika eneo hilo ambaye ataweza kuwathibitishia juu ya ukweli wa taarifa hizo.
Kwa mujibu wa msemaji wa waasi, shambulizi hilo lilifanyika katika mji huo wa Zlitan ambako miongoni mwa vikosi imara vya Kanali Gaddafi na ambacho kina vifaa vya hali juu kimejichimbia kuzuia waasi kusonga mbele kuelekea mji mkuu Tripoli.Mji huo wa Zlitan huko kiasi cha kilomita 160 kutoka Tripoli.
Khamis Gaddafi ambaye alipata mafunzo yake ya kijeshi nchini Urusi alikuwa akiongoza brigedi ya 32 ambayo inaogopewa sana.Waasi wiki hii walisema kuwa wamefanikiwa kuuthibiti mji huo wa Zlitan lakini serikali ya Libya ilikanusha madai hayo ya waasi.
Wakati huo huo televisheni ya Libya imearifu kuwa ndege za NATO mapema leo zimeshambulia mji mkuu Tripoli.
Imesema ndege hizo zimeshambulia makaazi ya raia na maeneo ya kijeshi huko kusini mashariki mwa Tripoli katika kitongoji cha Khellat al-Ferjan.
Mapema Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya Khaled Kaaim alisema kuwa waasi wamefanya hujuma dhidi ya bomba linalopeleka mafuta mjini Tripoli, kwa kuliziba na cement hali ambayo amesema itasababisha ukosefu wa umeme na uhaba wa nishati ya gesi mjini humo.
Amesema, chakula na madawa vimekuwa vikiharibika mjini humo kutokana na kutokuwepo kwa huduma ya umeme kwa muda mrefu, na kuongeza kuwa NATO wanataka kusababisha janga la kibinaadamu nchini Libya wakati ambapo wanadai kuwa harakati zao ni kuwalinda raia.
Wakati huo huo utawala wa Kanali Gaddafi unajaribu kuwagawanya waasi, kwa kudai kuwa umefikia makubaliano ya kuungana na wanaharakati wa kiislam.Kiongozi wa kundi hilo la wanaharakati wa kiislam Ali Sallabi amekri kuwa alifanya mazungumzo na mtoto wa Kanali Gadafi, Seif al-Islam, lakini amekanusha kama wamefikia makubaliano yoyote.
Waasi wa Libya ambao wanadhibiti eneo la mashariki mwa nchi hiyo,walikuwa katika hali ya kuparaganyika kufuatia kuawa kwa Jenerali Abdel Fatah Yunis.Waasi hao wamekuwa katika mbinyo mkubwa miongoni mwao kutaka kufanyika uchunguzi wa kina na wazi kuhusiana na mazingira ya kuawa kwa Jenerali Yunus.
Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/Reuters
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman