1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya watuma waangalizi 140 wa uchaguzi

George Njogopa30 Septemba 2015

Homa ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania imezidi kupanda huku waangalizi wa kimataifa wakianza kuwasili kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi huo unaotajwa kuwa wa kihistoria na wenye ushindani mkali.

https://p.dw.com/p/1Gg7M
Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya, Judith Sargentini, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2015.
Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya, Judith Sargentini, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2015.Picha: DW/G. Njogopa

Hii leo (Septemba 30), Umoja wa Ulaya umezindua rasmi timu ya waangalizi wake na kuahidi kufuatilia uchaguzi huo kwa kufuta misingi inayosimamia demokrasia ya kweli.

Waangalizi hao wanakuwa kundi ka kwanza kutoka jumuiya ya kimataifa kuwasili nchini na wameingia katika wakati ambapo shughuli za kampeni zikiingia hatua ya lala salama kwa wagombea kuendelea kunadi sera zao kwa wapiga kura.

Umoja wa Ulaya umepanga kusambaza kiasi cha waangalizi 140 watakaotawanyika katika maeneo mbalimbali huku tayari kundi la kwanza la waangalizi 32 likiwa limewasili. Kundi lingine linatarajiwa kutua nchini Oktoba 18.

Akizungunmza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mkuu wa ujumbe huo, Bi. Judith Sargentini, alisema waangalizi hao wapo nchini mwa mwaliko wa serikali ya Tanzania na tayari wamepata baraka kutoka tume zote mbili za uchaguzi.

Jukumu la waangalizi wa Ulaya

Mkuu huyo, ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Ulaya akitokea Uholanzi, alisisitiza pia waangalizi hao wakiwa nchini watazingatia kanuni na maadili kwa kuzingatia tamko la kimataifa kuhusu uchaguzi.

Waandishi wa habari na baadhi ya maafisa wa kibalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wakimsikiliza mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya, Judith Sargentini, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2015.
Waandishi wa habari na baadhi ya maafisa wa kibalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wakimsikiliza mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya, Judith Sargentini, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2015.Picha: DW/G. Njogopa

"Jukumu letu kubwa hapa ni kufutilia uchaguzi huu katika mazingira huru na kufanya tathmini ya kina kuhusu uchaguzi wenyewe na kuangalia ni kwa kiasi gani unashabiana na sheri zilizoko za Tanzania na zile za kimataifa", alisema.

Tayari ujumbe huo wa waangalizi umeshafanya mikutano kadhaa ikiwamo kukutana na vyama vyote vya kisiasa vinavyoshiriki uchaguzi wa mwaka huu, maofisa wa serikali na maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ya Zanzibar (ZEC).

Kwa hivi sasa vyama vyote viko katika pirikapirika za mwisho za kunadi sera zao majukwaani, huku mchuano mkali ukiwa baina ya mgombea wa CCM, John Magufuli, na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anayewania nafasi hiyo ya urasi kupitia CHADEMA chini ya mwamvuli wa muungano wa upinzani uitwao UKAWA.

Tafiti za kura za maoni zilizotolewa hivi karibuni zimetia joto uchaguzi huo na kuzusha mjadala mkubwa kwa wapiga kura. Uchaguzi wa mwaka huu unatarajia kuwavutia waangalizi wengi wa kimataifa hasa kutokana na ushindani uliopo ambao umeongezeka baada ya vigogo kadhaa wa chama CCM kutimkia upinzani.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef