Afghanistan Wahlablauf
21 Agosti 2009Waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi wa Afghanistan wameridhika na jinsi uchaguzi huo ulivyofanyika, licha ya kitisho kilichotolewa na wapiganaji wa Taliban kutaka kuuvuruga.
Tume huru ya uchaguzi ya Afghanistan inasema idadi kubwa ya watu walijitokeza kupiga kura zao katika uchaguzi huo wa jana. Hata hivyo mwenyekiti wa tume hiyo, bwana Aziz Ludin, anasema bado ni mapema kutaja idadi kamili ya waliopiga kura.
"Uchaguzi umefanyika vizuri na natumai idadi kubwa ya Waafghanistan wameshiriki." Kura zao zitachangia kuboresha hali ya nchi yao katika siku za usoni na kuimarisha mfumo mpya wa kisiasa nchini Afghanistan."
Kwa tathmini yake bwana Ludin Aziz amesema uchaguzi huo wa pili wa urais na mikoa kwa ujumla umefanyika kwa njia huru ya haki. Amesita lakini kuthibitisha hilo kwani Afghanistan ni taifa kubwa na bado hajapokea habari kamili kutoka vituo vyote takriban 6,200 nchini kote.
Wakala wa Afghanistan unaopigania uchaguzi huru na wa haki, umeonya kwamba ni mapema mno kutoa tathmini ya uchaguzi wa jana kwani habari zitaendelea kufichuka kati ya siku moja hadi mbili baada ya uchaguzi huo kufanyika.
Kai Eide ni kiongozi wa tume ya Umoja wa Mataifa iliyokwenda kusaidia kuratibu shughuli za uchaguzi nchini Afghanistan, UNAMA. Anasema licha ya mashambulio yaliyofanywa na wapiganaji nchini Afghanistan kujaribu kuvuruga uchaguzi wa jana, wamepata mafanikio.
" Watu wengi walijiuliza ikiwa kweli uchaguzi huu ungefanyika. Tumeshuhudia kutokea kwa mashambulio ya hapa na pale, lakini hata hivyo uchaguzi umefanyika kwa utaratibu mzuri. Takriban vituo 6,200 vya kupigia kura vilikuwa wazi. Hicho ndicho kilichokuwa kigezo changu cha ufanisi wa uchaguzi huu. Naamini hii ni siku nzuri kwa Afghanistan."
Mwadiplomasia huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan amewapongeza Waafghanistan kwa kusaidia kufanikisha uchaguzi nchini mwao. Bwana Kai ameongeza kusema na hapa namnukulu, "Nawapongeza Waafghanistan wote waliokuwa na wasiwasi kuhusu uratibu na usalama wakati wa uchaguzi. Nawapongeza watu wote waliojitokeza kupiga kura ili kuzipiga jeki juhudi za kuiimarisha demokrasia", mwisho wa kumnukulu kiongozi huyo wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA.
Waangalizi wengi huria nchini Afghanistan wameshangazwa na jinsi watu walivyojitokeza kupiga kura. Wengi wao wanaamini kutokana na machafuko yanayoikabili nchi hiyo na shinikizo kubwa la wanamgambo wa kundi la Taliban, vituo vingi vya kupigia kura vilikuwa vitupu.
Mshindi wa uchaguzi wa jana atatangazwa rasmi katika kipindi cha wiki mbili zijazo. Hadi kufikia wakati huo, Waafghanistan na ulimwegnu mzima kwa jumla unabakia ukibahatisha ni nani atakeyeiongoza Afghanistan kati ya rais wa sasa Hamid Karzai na mpinzani wake Dr Abdullah Abdullah.
Mwandishi:Shamel, Ratbil (DW Afghanisch) , NEU
Mhariri: Abdul-Rahman