Waandamanaji wavuruga shughuli za uokoaji nchini Haiti.
18 Novemba 2010Migomo imekithiri nchini Haiti na raia wa kisiwa hicho wanaendelea kuwashambulia wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaolaumiwa kwa kusababisha kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu.
Mtu mmoja alifariki baada ya kupigwa risasi na wengine walijeruhiwa kaskazini mwa kisiwa cha Haiti ambapo maafisa wa afya wanadai mkurupuko wa kipindupindu unaweza kusababisha vifo vya takriban watu 10,000.
Wizara ya afya nchini humo imesema kwamba kiasi ya watu 1,100 wamefariki kutokana na maambukizi ya ugonjwa huo ulioanza mwishoni mwa mwezi Oktoba. Idadi ya waathiriwa waliolazwa hospitalini imefikia 18,382. Mshauri wa shirika la afya la Kimarekani, Ciro Ugarte ameliambia shirika la habari la AFP kwamba makadirio yao yanaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja ujao, kutakuwa na visa laki mbili vya maambukizi ya kipindupindu nchini Haiti. Mshauri huyo ameonya kwamba ikiwa kiwango cha maambukizi kitaendelea kuwa kati ya asilimia nne au tano, huenda watu 10, 000 wakafariki.
Visa vichache vya maambukizi ya ugonjwa huo vimeripotiwa katika Jamhuri ya Dominica. Wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wanalalamika kwamba maandamano hayo yanavuruga jitihada za kusambaza misaada hasa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Cap Haitien. Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba maandamano hayo yanaonekana yamepangwa.
Raia wawili waliuliwa kwa kupigwa risasi katika mji wa Cap Haitien siku ya Jumatatu. Mmoja wao alifyatuliwa risasi na mwanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, alipojaribu kukiteketeza kituo cha polisi na kutoa kitisho cha kuteketeza pia afisi za Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Umoja huo, Vincenzo Pugliese hajathibitisha ikiwa kuna mwanajeshi wa umoja huo aliyeuawawa lakini amesema kwamba wafanyakazi wa umoja huo hawakwenda kazini jana kutokana na hali ya wasi wasi iliyotanda katika mji mkuu.
Msemaji mwingine wa shirika la kutoa misaada la Oxfam, Julie Schindall amethibitisha kwamba barabara zimefungwa na waandamanaji kwa kutumia magurudumu na wafanyakazi wengi hawawezi kwenda kazini hasa kusambaza bidhaa muhimu kama sabuni na madawa. Afifa mmoja wa maafisa wa Umoja wa Mataifa amesema katika kisa kingine wiki hii, ghala la shirika la chakula duniani, WFP lilivunjwa na zaidi ya tani 500 ya chakula ikaporwa.
Mkurupuko wa kipindupindu ambao ni wa kwanza katika kipindi cha miongo mitano katika kisiwa hicho maskini, kilichoko katika eneo la Caribbean, unasababisha matatizo makubwa hasa baada ya tetemeko la ardhi la mwezi Januari lililowauwa watu 250,000 na kuwaacha mamilioni ya raia bila makaazi.
Kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani nchini humo, MINUSTAH kimetoa taarifa inayohusisha maandamano hayo na uchaguzi mkuu na kimetoa mwito kwa Wahaiti wasitumiwe vibaya na maadui wa utulivu na demokrasia.
Mwandishi: Peter Moss / AFP
Mhariri:Yusuf Saumu Ramadhan